Fumbo la uvumilivu wa Mungu linajionesha katika hija ya maisha ya mwanadamu!
Mwenyezi Mungu anatumia njia mbali mbali ili kuingia kwenye historia ya maisha ya
mwanadamu, wakati mwingine anatekeleza mpango wake kwa taratibu, lakini jambo la msingi
ni kujenga na kukuza fadhila ya imani na udumifu, bila ya kukata tamaa. Abrahamu alipoambiwa
kwamba, angekuwa ni Baba wa Mataifa, alishangaa sana kwani walikuwa wamekwisha kula
chumvi ya kutosha na kwa umri wao walikuwa hawategemei tena kupata mtoto!
Katika
mazingira kama haya kuna haja kwa waamini kuwa wavumilivu na wadumivu katika maisha
ya sala, kwani Mwenyezi Mungu anaendelea kumsubiri binadamu hadi hatima ya maisha
yake. Kuna baadhi ya watu walibahatika kukutana na Kristo katika dakika za mwisho
wa maisha yao!
Yule mwizi aliyekuwa ametundikwa Msalabani pamoja na Yesu pale
Mlimani Kalvari, alimgundua Mwenyezi Mungu katika dakika za mwisho mwisho wa maisha
yake. Hivi ndivyo ilivyotokea kwa wale Wanafunzi wa Emmaus. Wakati mwingine mwamini
anasahau kwamba, Mwenyezi Mungu anafanya hija pamoja naye katika maisha, hata pale
wanaposahau, bado Mwenyezi Mungu anaonesha uvumilivu mkuu.
Hii ni sehemu ya
mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya
Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae, kilichoko mjini Vatican,
siku ya Ijumaa, tarehe 28 Juni 2013. Baba Mtakatifu amewatafakarisha haya viongozi
waandamizi na wafanyakazi kutoka Idara ya Afya ya Vatican kuhusu Fumbo la uvumilivu
wa Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha ya mwanadamu.
Kuna wakati ambapo mwamini
anakumbana na giza pamoja na utupu katika maisha yake ya kiimani, hapo ndipo anapotamani
kushuka kutoka kwenye Msalaba, kwani amekosa uvumilivu! Haya ndiyo waliyokuwa wanamwambia
Yesu alipokuwa pale juu ya Msalaba, lakini aliwaonesha uvumilivu wa ajabu hadi chembe
ya mwisho ya maisha yake, alipoinamisha kichwa, akakata roho!
Baba Mtakatifu
Francisko anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema ili aweze kufanya hija
ya maisha pamoja nao, kama inavyojionesha katika maisha ya Abraham bila ya kukata
tamaa!