Jamhuri ya Afrika ya Kati ni taifa ambalo linaendelea kupoteza dira na mwelekeo wa
maisha, kiasi kwamba, ile misingi ya haki, amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa
vinatoweka taratibu kutokana na vita inayoendeshwa na Kikosi cha Waasi wa Seleka,
baada ya mapinduzi ya Serikali yaliyofanyika kunako tarehe 24 Machi 2013.
Hayo
yamebainishwa na Askofu mkuu Diudonnè Nzapalainga, wa Jimbo kuu la Bangui. Kikosi
cha Waasi wa Seleka kimekuwa kikiendelesha madhulumu ya kidini dhidi ya Wakristo pamoja
na kusababisha watu kukimbia maeneo yao kutokana na kukosekana kwa misingi ya haki,
amani na utulivu. Hii ni changamoto kwa viongozi mbali mbali wa kisiasa na kidini
kukaa pamoja ili kujadili hatima ya maisha ya wanachi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.