Caritas na mikakati ya msaada wa dharura kwa waathirika wa vita nchini Mali
Kamati tendaji ya Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Mali, imehitimisha
kikao chake cha siku mbili, kilicho jadili pamoja na mambo mengine, utoaji wa msaada
wa dharura kwa watu walioathirika kwa migogoro na vita Kaskazini mwa Mali. Wajumbe
wa kamati wamezungumzia kuhusu upatikanaji wa fedha zitakazogharimia miradi mbali
mbali inayoendeshwa Kaskazini mwa Mali.
Kwa pamoja, Mali imeamua kushirikiana
na Mashirika mengine manne ya Caritas Ukanda wa Sahel unaojumuisha nchi za: Burkina
Faso, Niger, Senegal na Mali yenyewe. Mashirika mengine ya misaada yanayochangia gharama
kwa kiasikikubwa ni Caritas Italia, Caritas Hispania na Shirikisho la Misaada ya Kanisa
Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis.
Msaada huu unawalenga hasa watu
wasiokuwa na makazi maalum, wakimbizi na Jumuiya ambazo zimeathirika na vita nchini
Mali. Caritas Ukanda wa Sahel itawezeshwa ili kukabiliana na changamoto hizi katika
kuratibu na mambo ya mawasiliano ili Caritas iweze kutoa huduma bora zaidi kwa walengwa.