Waislam na Wakristo wanayo dhamana ya kulinda na kutetea maisha ya kiroho, maadili
na utu wema!
Tume ya pamoja kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikatoliki, hivi karibuni, imehitimisha
mkutano wake wa mwaka uliokuwa chini ya uongozi wa Kardinali Jean Louis Tauran, Rais
wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Katika mkutano huu, ujumbe kutoka kwa
waamini wa dini ya Kiislam uliongozwa na Professa Hamid Bin Ahmad Al Rifaie, Rais
wa Jukwaa la Kimataifa la dini ya Kiislam kwa ajili ya majadiliano ya kidini.
Katika
majadiliano yao ya pamoja, wametambua na kuridhia umuhimu wa mambo ya kiroho na maisha
ya kidunia, wajibu kwa waamini wa dini hizi mbili ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi
kuweka uwiano mzuri katika masuala haya mintarafu mwelekeo wa maisha. Watu wengi duniani
wanakabiliana na mmong'onyoko wa tunu msingi za maisha ya kiroho na kimaadili, mwaliko
kwa waamini wa dini hizi mbili kuwalinda na kuwatetea wanyonge katika hali kama hizi
kwa kukazia maadili na utu wema.
Wajumbe hawa wamekubaliana kimsingi kwamba,
leo hii kuna aina nyingi za kinzani na migogoro, wajibu wao kama waamini ni kuwalinda
watu wanaokabiliwa na hali kama hizi. Wajumbe hawa wanasema walipata nafasi ya kuweza
kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, aliyewahimiza kuendeleza dhamana
hii nyeti kwa kuheshimiana na kuthaminiana ili majadiliano miongoni mwa waamini wa
dini hizi mbili yaweze kuzaa matunda ya amani, ustawi na maendeleo endelevu.
Wajumbe
katika ujumla wao, wamelaani vita inayoendelea nchini Syria na hivyo kupelekea mauaji
ya watu wasiokuwa na hatia, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha utakatifu wa maisha
ya binadamu. Wajumbe wanapenda kutoa mwaliko kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa
kuongeza juhudi zaidi ili kuweza kupata suluhu ya mgogoro wa Syria na hivyo kusitisha
mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Wajumbe wa Tume hii ya pamoja, wamekubaliana
kwamba, watakutana tena kwa mkutano mwingine, utakaofanyika mjini Tatwan, Morocco,
lakini utatanguliwa na maandalizi na kwamba, mkutano huu utaandaliwa na upande wa
waamini wa dini ya Kiislam.