Shukrani kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania! Maaskofu wanaalikwa kuendelea kuwa
ni sauti ya Kinabii kwa kusimamia Ukweli!
Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro anapomshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kumwezesha kusherehekea Jubilee ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu wa
Jimbo la Tanga na baadaye Jimbo Katoliki la Morogoro, anamshukuru Mwenyezi Mungu,
Maaskofu na Watanzania katika ujumla wao.
Kwa namna
ya pekee anapenda kuwashukuru Maaskofu wenzake, ambao wameonesha moyo wa upendo, umoja
na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na watanzania katika ujumla
wao! Askofu Mkude ameyasema hayo wakati wa mahojiano maalum na Radio Vatican katika
Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kama Askofu, sanjari na
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yaani hii ni zawadi mara mbili!
Matunda ya mshikamano
na umoja huu ambao ni baraka na neema ya Mungu yanajionesha kwa namna ya pekee katika
huduma zinazotolewa na Kanisa Katoliki katika sekta mbali mbali za maisha ya watanzania:
katika afya, lakini zaidi katika elimu. Kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha
Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT, ilikuwa ni kati ya changamoto kubwa iliyofanyiwa
kazi na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Leo hii SAUT imekuwa na kupanuka na
ni kati ya Vyuo vikuu nchini Tanzania yenye wanafunzi wengi na iliyoeneza matawi yake
sehemu mbali mbali za Tanzania.
Askofu Mkude anasema, si kwa bahati mbaya kwamba,
Baraza la Maaskofu Katoliki liliamua kukipatia Chuo Kikuu cha Kikatoliki jina la Mtakatifu
Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, kwani walitaka wanafunzi watakaobahatika kusoma
katika Chuo hiki waweze kujitoa bila ya kujibakiza katika ujenzi wa "Mji wa Mungu";
wajitoe kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu.
Hii ndiyo furaha ya Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema Askofu Mkude na kwamba ni matunda ya mshikamano,
umoja na sala, changamoto ya kusonga mbele kwa imani na matumaini thabiti.
Askofu
Mkude anasema, Maaskofu wanapaswa kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii nchini Tanzania
kwa kusema na kutetea ukweli, hata ikiwa ni lazima watoe sadaka kubwa, kwani ukweli
utawaweka huru! Ukweli huu usemwe katika medani mbali mbali ya maisha ya watanzania,
kwani watu wanatarajia kusikia msimamo wa Kanisa katika masuala mbali mbali yanayogusa
maisha yao.
Ni wajibu kwa Kanisa kuendelea kutoa mwanga utakaowawezesha waamini
na wananchi kujipima mbele ya Mwenyezi Mungu na Jamii inayowazunguka; pale walipokosea,
waweze kutubu na kufanya marekebisho! Pale walipofanikiwa, basi wamshukuru Mungu.
Maaskofu wanayodhamana ya kuliombea Kanisa na Tanzania katika ujumla wake; wana dhamana
ya kulielekeza Kanisa na Watanzania; kuwatia ari na moyo, kuwapa mwanga na faraja
kwani Kanisa ni Mama wa wote.
Askofu Telesphor Mkude katika mahojiano maalum
na Radio Vatican anaendelea kuiombea Tanzania: haki, amani, upendo, mshikamano, ustawi
na maendeleo endelevu!