Mkusanyiko wa Katekesi za Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ni utajiri mkubwa katika
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani
Idara ya Uchapaji ya Vatican imechapisha kitabu ambacho ni mkusanyiko wa Katekesi
za Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika Maadhimisho ya Mwaka wa
Imani, tangu tarehe 10 Oktoba 2012 hadi tarehe 27 Februari 2013 siku moja kabla ya
kung’atuka kutoka madarakani kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kupata nafasi ya
kupanda kwenda Mlimani kwa ajili ya kutafakari na kusali kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya Kanisa la Kristo.
Kitabu hiki
cha Mkusanyiko wa Katekesi za Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kina utajiri mkubwa wa sanaa zinazoonesha Kanuni ya
Imani katika michoro maarufu. Huu ni utajiri unaonesha kwa namna ya pekee Maadhimisho
ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ambalo limekuwa ni tukio kubwa katika maisha na
utume wa Kanisa katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Mwaka wa
Imani ni mwaliko kwa Waamini kuwa na ari na mwamko mpya katika: kuifahamu, kuiadhimisha,
kuimwilisha katika maisha adili pamoja na kuisali kama sehemu ya mchakato wa ushuhuda
wa imani tendaji. Ni changamoto ya kuendelea kumtangaza Yesu Kristo kuwa kweli ni
Mkombozi wa Ulimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha unaoonesha umuhimu wa imani kwa
Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika katekesi
zake kwa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani amejaribu kujibu swali la msingi imani ni kitu
gani kwa mwamini katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia?
Ameangalia umuhimu wa imani inayoungamwa na Jumuiya ya Wakristo; kiu ya kumfahamu
Mwenyezi Mungu na hamu ya kutaka kumpeleka katika moyo wa mwanadamu! Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Katekesi zake anajaribu kumwonesha mwamini
jinsi anavyoweza kumfahamu mwenyezi Mungu, maana ya ufunuo unaojionesha kwa namna
ya pekee katika upendo unaojikita katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Anaonesha
nafasi ya Bikira Maria katika imani, kwa kuanzia katika Fumbo la Umwilisho, Bikira
Maria ni Mama aliyeonesha utii wa imani. Nafasi ya Roho Mtakatifu, Kanuni ya Imani
ni mambo ambayo mwamini anapaswa kuyafahamu kwa kina kama sehemu ya hija yake ya imani
hapa duniani.
Baba Mtakatifu amegusia pia vishawishi ambavyo Yesu alikutana
navyo alipokuwa Jangwani. Kwa hakika, Mwaka wa Imani unapania kuwaimarisha waamini
katika imani yao kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati. Kila mtu
anapaswa kutambua na kuonja kwamba, anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu ndiyo
maana akamtuma Mwanaye wa Pekee yesu Kristo aweze kuja ulimwenguni, akabiliane na
mateso, kifo na hatimaye, siku ya tatu kufufuka kutoka katika wafu ili kumkomboa mwanadamu
kutoka katika lindi la dhambi mauti.
Ni changamoto kwa kila Mkristo kusikia
ile furaha ya kuwa kweli ni mfuasi wa Kristo ili hatimaye, aweze kuitolea ushuhuda
wa kweli katika uhalisia wa maisha.
Imani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu na hakuna mtu anayeweza kuipokonya, lakini inapaswa kurutubishwa kwa: sala,
tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya Huruma yanayoonesha
imani katika matendo.