Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani anaendelea kulichambua Kanisa kama Familia ya Mungu, mintarafu Kanuni ya
Imani. Jumatano, tarehe 26 Juni 2013 ametafakari kuhusu Kanisa kama Hekalu la Roho
Mtakatifu. Kristo alilinunua kwa damu yake azizi, akalijaza Roho wake na kulijalia
misaada inayofaa kwa ajili ya umoja uonekanao na wa kijamii.
Baba Mtakatifu
anasema, Hekalu la Selemani lililoko Mjini Yerusalem, mahali ambapo waamini walikutana
na Bwana, lilikuwa ni kielelezo cha Kanisa. Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyetwaa mwili
anaishi ndani mwa waamini wake, Yeye kimsingi ndiye Hekalu hai, mahali ambapo waamini
wanaweza kukutana na Mwenyezi Mungu.
Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo
anawapatia uwezo waamini kuwa ni mawe hai na sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani
Kanisa. Hapa ni mahali ambapo waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanatekeleza
dhamana ya ukuhani wao kwa kutolea sadaka takatifu ya maisha ya kiroho.
Baba
Mtakatifu anasema kwamba, Roho Mtakatifu kwa njia ya karama na mapaji mbali mbali
anayowakirimia waamini, anawaunganisha na hivyo kuwawezesha pia kuchangia katika ujenzi
wa utakatifu wa Kanisa. Katika utekelezaji wa dhamana hii kubwa anasema Baba Mtakatifu,
kila mtu anapaswa kushiriki, kwa kutambua kwamba, ni jiwe hai na lenye thamani katika
kupamba Hekalu la Mungu.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali ili kwamba,
kila mmoja wao aweze kutekeleza wajibu wake katika maisha na utume wa Kanisa, kwa
kuongozwa na Roho Mtakatifu na kuwa, Yesu Kristo ndiye Jiwe kuu la Msingi. Baba Mtakatifu
ametambua uwepo wa mahujaji wanaozungumza lugha ya Kiingereza, kati yao ni wale waliotoka
Afrika ya Kusini.
Roho Mtakatifu awajaze moyo wa upendo na ari mpya, ili waweze
kuishi kwa kufuata mfano wa Kristo. Anawakumbusha kwamba, mchoko na hali ya kukata
tamaa itawafanya kushindwa kuwa kweli ni mawe hai na matokeo yake watajikuta wamejitenga
na Kristo. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema ni matumaini yake kwamba, mkutano wa katekesi
yake utawatia nguvu na ari ya kutangaza Habari Njema ya wokovu iliyoletwa na Yesu
Kristo.