Ulimwengu unahitaji kuona ushuhuda wa pamoja unaotolewa na waamini wa dini mbali mbali
katika kulinda, utu, heshima, haki na amani duniani!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 24 Juni 2013 amekutana na kuzungumza na
ujumbe wa Tume ya Wayahudi ya Majadiliano ya Kidini Kimataifa, uliomtembelea mjini
Vatican. Kwa takribani miaka arobaini, Kanisa Katoliki limekuwa likifanya majadiliano
ya kidini na Wayahudi, hali ambayo imechangia kuimarika kwa urafiki kati ya waamini
wa dini hizi mbili.
Tume hii inatarajiwa kufanya tena mkutano wake mwezi Oktoba,
2013 mjini Madrid, Hispania kwa kuongozwa na kauli mbiu "Changamoto za kiimani katika
Jamii mamboleo". Baba Mtakatifu Francisko anasema, tangu aanze kutekeleza utume wake
kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amebahatika kukutana na kuzungumza na viongozi mbali
mbali wa dini ya Kiyahudi, lakini kwa mara ya kwanza amezungumza rasmi na Tume hii.
Kwa upande wa Kanisa Katoliki, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican umekuwa ni
msingi rejea wa majadiliano ya kidini na kwa namna ya pekee na waamini wa dini ya
Kiyahudi kwamba, kuna cheche za imani kutoka kwa Mababu na Manabii wanazoshirikishana.
Baba Mtakatifu amelaani vitendo vya chuki, madhulumu na ubaguzi unaofanywa kwa misingi
ya kidini na kusema kwamba, mizizi ya imani ya dini hizi mbili haiwezi kuruhusu msimamo
kama huu!
Misingi mikuu ya imani iliyobainishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa
Pili wa Vatican imekuwa ni dira na kielelezo cha majadiliano baina ya waamini wa dini
hizi kama sehemu ya mchakato wa kufahamiana na kuthaminiana, hali ambayo imejionesha
kwa namna ya pekee katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Kumekuwepo na nyaraka
mbali mbali zinazobainisha misingi ya uhusiano wa kitaalimungu kati ya Wayahudi na
Wakristo, jambo ambalo waamini wanapaswa kumshukuru Mungu.
Baba Mtakatifu anasema
kwamba, majadiliano ya kidini na Wayahudi ni jambo ambalo linaendelea kuota mizizi
yake hata katika Makanisa mahalia, kama alivyojitahidi kutekeleza wakati alipokuwa
Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires. Alipata nafasi ya kujadiliana kwa kina na
mapana kuhusu utambulisho wao wa kidini, sura ya binadamu mintarafu Maandiko Matakatifu;
jinsi ya kuuhisha uwepo wa Mungu kati ya walimwengu waliokengeuka na pamoja na jinsi
ambavyo waamini wa dini hizi mbili wanavyoweza kupambana na changamoto za kiimani.
Jambo
kubwa zaidi anasema Baba Mtakatifu ni ile hali ya kuthamini uwepo wao, majadiliano,
ukarimu na kusaidiana kwa hali na mali kama waamini. Urafiki kati ya watu ni msingi
thabiti wa majadiliano ya kidini, changamoto ya kuwahusisha vijana wa kizazi kipya.
Ulimwengu unahitaji kuona ushuhuda wa pamoja unaotolewa na waamini wa dini mbali mbali
duniani katika kulinda, kudumisha na kutetea utu na heshima ya binadamu, haki na amani
ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.