2013-06-25 09:21:02

Madhara ya vita ya wenyewe kwa wenyewe Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati!


Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Afrika ya kati hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa Mwaka kwa kuelezea hali ngumu ambayo wananchi wa Afrika ya Kati wamekumbana nayo wakati wa machafuko ya kisiasa na vita baada ya Kikundi cha Waasi cha Seleka kupindua Serikali na kujitwalia madaraka hapo tarehe 24 Machi 2013.

Maaskofu wanasema watu wengi wamepoteza maisha na mali zao kutokana na vita hii na kwamba, bado watu wana wasi wasi na usalama wa maisha yao. Msingi wa maisha ya Kijamii na Kifamilia umetikiswa kwa kiasi kikubwa, kiasi kwamba, watu wengi wamesambaratika. Inasikitisha kuona kwamba, rasilimali na utajiri wa nchi vimebinafsishwa kwa ajili ya mafao ya watu wachache katika Jamii wakati ambapo mamillioni ya wananchi yanaendelea kuteseka kwa njaa, magonjwa na umaskini.

Hali ya kisiasa si shwari kwani kumbu kumbu nyingi zimeharibiwa bnaada ya Kikundi cha Waasi wa Seleka kuchoma moto Masjala ya Taifa. Hili ni tukio ambalo limefuta kumbu kumbu nyeti za taifa, kiasi cha kuhatarisha usalama wa taifa. Baraza la Maaskofu bado linaonesha masikitiko yake kutokana na vita kuharibu kabisa mfumo wa masomo, kwa sasa wanaendelea kutafakari nini cha kufanya kuhusu hatima ya maisha ya wanafunzi hawa.

Licha ya kutwaa madaraka kwa nguvu bado Kikundi cha Seleka kinajitambulisha kuwa ni Jeshi la waasi kwa kukosa kanuni na sheria maadili ya kazi na kwamba, maisha kwao si tena kitu cha thamani, kinachopaswa kulindwa na kuheshimiwa! Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, wananusa damu kila siku ya maisha yao kwa sasa! Hii ndiyo gharama ya vita ambayo haina pazia! Maaskofu wanalaani kwa nguvu zao zote kitendo cha kuwaandaa watoto na kuwapeleka mstari wa mbele kupigana ni jambo ambalo linatisha kwani linawanyima watoto hao haki zao msingi na kuwaharibia maisha kwa sasa na kwa siku za usoni.

Maaskofu wameangalia pia athari kubwa zilizosababishwa na Vikosi vya Jeshi la Waasi wa Seleka katika Makanisa na kusema, nyumba nyingi za Ibada zimenajisiwa, changamoto kwa waamini kutokatishwa tamaa na vitendo hivi, bali wasimame kidete kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wanachangamotishwa na Maaskofu wao kusonga mbele kwa ari kubwa zaidi ili kutangaza Injili ya Upendo, Msamaha na Upatanisho. Imani yao ijioneshe katika medani mbali mbali za maisha, daima wakisimama kidete kulinda na kutetea: utu na heshima ya binadamu, haki msingi na mafao ya wengi.

Waamini wakatae kabisa vitendo vya rushwa na ufisadi; ukabila na upendeleo; wasimamie demokrasia, haki na utawala wa sheria. Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Wananchi wa Afrika ya Kati linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupiga moyo konde na kuanza mchakato wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho wa kweli; kwa kukazia majadiliano katika haki na ukweli.

Mchakato huu unapaswa kuwahusisha pia viongozi wa dini mbali mbali ili kuondoa ile hali ya kudhaniana vibaya na badala yake kujenga umoja, upendo, udugu na mshikamano miongoni mwa wananchi wote na kwamba, tofauti zao za kiimani, kidini na kikabila ni utajiri mkubwa unaopaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya watu wao!







All the contents on this site are copyrighted ©.