Maadhimisho ya Mwaka wa Imani: Siku ya Familia: 26 hadi 27 Oktoba 2013
Baraza la Kipapa la Familia limeanza kuandikisha majina ya familia ambazo zinapenda
kushiriki katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kwa kutembelea Kaburi la Mtakatifu
Petro katika kilelle cha Maadhimisho haya kwa Familia hapo tarehe 26 hadi 27 Oktoba
2013 hapa mjini Vatican. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu "Familia inaishi
furaha ya imani!
Hii itakuwa ni fursa makini kwa Familia kutoka sehemu mbali
mbali za dunia kuweza kukutana pamoja kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
ili kusali, kutafakari na kushirikishana furaha ya imani inayobubujika kutoka kwa
Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Ni muda wa kutolea ushuhuda wa nguvu tunu msingi za
maisha ya kifamilia na utu wema. Wanafamilia watapata nafasi nyingine tena ya kugundua
umuhimu wa Familia kama mahali muafaka pa kurithisha imani ya Kikristo.
Katika
Maadhimisho haya, watoto wenye umri kati ya miaka 3 hadi 12 wanaalikwa kutuma michoroinayohusiana
na Familia zao; michoro ambayo itawasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko, ili kujionea
ufahamu wa watoto kuhusiana na Familia zao. Watoto wenye umri kati ya miaka 13 hadi
18 wataweza kuwashirikisha wengine picha za familia zao kwa kutuma kwenye mtandao
wa Baraza la Kipapa la Familia. Vijana wenye karama na vipaji mbali mbali watashiriki
pia katika tamasha linaloonesha karama na vipaji vya familia.
Ratiba elekezi
kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa Familia inaonesha kwamba, tarehe 26
Oktoba, Familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia zitapata nafasi ya kuungama ili
kuweza kupokea rehema na neema zinazotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani. Mchana Familia hizi zitakutanika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro. Jioni, Familia zitasali kwa pamoja na baadaye zitaungana na Baba Mtakatifu
Francisko ili kukiri imani kwa pamoja.
Kilele cha Maadhimisho haya ni hapo
Jumapili, tarehe 27 Oktoba. Saa 3: 30, Familia zitasali na kutafakari kwa pamoja Rozari
Takatifu; muhtasari wa Injili na baadaye zitajiunga na Baba Mtakatifu kwa ajili ya
Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, inayotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko
pamoja na kusali kwa pamoja Sala ya Malaika wa Bwana.