Kanisa nchini Pwani ya Pembe linajielekeza zaidi katika Uinjilishaji Mpya!
Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe hivi karibuni limehitimisha mkutano wake
wa kawaida wa tisini na sita uliochambua pamoja na mambo mengine: hali ya uchumi na
fedha katika Kanisa na Taasisi zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki nchini
humo; mikakati na sera za maendeleo ya Kanisa, lakini zaidi changamoto ya Uinjilishaji
Mpya; mkakati wa kichungaji unaopewa kipaumbele cha pekee na Mama Kanisa katika mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Maaskofu wanamshukuru
Mwenyezi Mungu kwa yale yote ambayo wamefanikiwa kuyatekeleza kama sehemu ya Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani. Kanisa limetoa mchango makini katika jitihada za kulinda na kudumisha
misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa, mara baada ya kutokea machafuko ya
kisiasa nchini humo kunako mwaka 2010.
Padre Roberto Campisi, afisa kutoka
Ubalozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe, amewachangamotisha Maaskofu Katoliki kuwekeza
zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, katika mapambazuko ya Millenia ya tatu
ya Ukristo, kwa kutoa fursa kubwa zaidi kwa waamini walei kushiriki katika maisha
na utume wa Kanisa, kwani wao wanatumwa ulimwenguni kuyatakatifuza malimwengu kwa
njia ya ushuhuda wa maisha yao adili.
Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya
Pembe, limeanzisha Tume ya Uinjilishaji Mpya, itakayobainisha sera na mikakati itakayotumiwa
na Maaskofu katika utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji nchini humo, kwa kuwaendea
wale ambao kwa miaka ya hivi karibuni wamelegea na kuanza kusinzia katika imani.
Maaskofu
wameamua pia kuanzisha Mfuko wa kulitegemeza Kanisa nchini humo kama sehemu ya changamoto
iliyotolewa na Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika. Hili ni tatizo kubwa
linaloendelea kukwamisha shughuli na mikakati ya maendeleo kwa Makanisa mengi Barani
Afrika.
Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Mwaka wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Pwani ya Pembe, ilikuwa ni fursa pia ya kuweza kusikiliza kwa makini taarifa mbali
mbali zilizotolewa na Wakuu wa Idara na Tume za Baraza la Maaskofu Katoliki; mafanikio,
matatizo, fursa na changamoto zilizoko mbele yao. Mkutano mkuu wa 97 unatarajiwa kufanyika
mwezi Januari 2014, kwenye Jimbo kuu la Gagnoa.