2013-06-25 10:42:07

Kanisa linatumwa kuhudumia, kupenda na kuthamini maisha ya watu!


Mama Kanisa anatumwa kuhudumia, kupenda na kumwamini mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni nguzo kuu tatu za mafundisho ya Mtumishi wa Mungu Papa Paulo wa sita, katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ni kiongozi aliyeshuhudia imani yake kwa Kristo na Kanisa katika mazingira magumu, lakini akathubutu kuonesha upendo wake kwa Kristo. Ilikuwa ni hamu ya moyo wake, kuhakikisha kwamba, Habari Njema ya Wokovu inahubiriwa hadi miisho ya dunia. Yesu Kristo anapaswa kuwa ni kiini cha maisha na utume wa kila mwamini.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni, alipokutana na waamini zaidi ya elfu tano kutoka Brescia, Kaskazini mwa Italia, waliofika mjini Vatican kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, sanjari na kumbu kumbu ya miaka hamsini tangu Papa Paulo wa Sita alipochaguliwa kuliongoza Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, Papa Paulo VI ni kiongozi aliyeonesha upendo wa hali ya juu kwa Kanisa, kama inavyojidhihirisha katika Waraka wake wa kichungaji "Kanisa la Kristo", "Ecclesiam Sua". Hiki ni kiini cha moyo na utume wake kama Mchungaji mkuu wa Kanisa, aliyependa kuliona Kanisa likijimwaga ulimwenguni kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo. Alitambua kwamba, Kanisa lina fadhila ya kimama, inayowaongoza waamini kwa Kristo, changamoto kwa waamini kuhakikisha kuwa wanashikamana na Kristo katika hija ya maisha yao hapa duniani; tayari kuwakumbatia wale wote wanaoishi pembezoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Papa Paulo VI alionesha upendo mkuu kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwanadamu anapaswa kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa. Alipenda kuonesha ile sura ya Msamaria mwema katika kukabiliana na changamoto kutoka kwa watu waliokuwa wamemezwa na malimwengu! Alipenda kuwahudumia wote hawa kwa moyo wa upendo na unyenyekevu mkuu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Kanisa ni mhudumu na mlinzi wa maisha ya binadamu.

Kanisa linapokabiliana na changamoto za ukanimungu, linapaswa kukumbuka mafundisho ya Papa Paulo VI kwamba, Kanisa linamwamini Kristo aliyetwaa mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu, akakaa kati ya watu wake na kuwa sawa nao katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi. Huu ni urithi mkubwa wa Mafundisho ya Papa Paulo VI kwa Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu aliwataka waamini kutoka Brescia, kuendelea kumuenzi Papa Paulo VI kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao ndani na nje ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba, kabla ya kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, waamini kutoka Brescia waliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Luciano Monari wa Jimbo Katoliki Brescia.







All the contents on this site are copyrighted ©.