Serikali ina wajibu wa kusikiliza kilio cha raia wake! Lakini vurugu hapana!
Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linasema, limekuwa likifuatilia kwa karibu zaidi
matukio yanayoendelea kutokea nchini humo kuhusiana na kupanda kwa gharama za maisha
na kuzorota kwa hali ya maisha kutokana na mchakato wa maandalizi ya Kombe la Dunia,
litakalofanyika nchini Brazil hapo mwakani. Maaskofu wanapenda kuonesha mshikamano
wao wa upendo na wananchi kwa wote wanaoshiriki katika maandamani ya amani kama njia
ya kushirikisha mawazo na wasi wasi wao!
Kuna haja kwa wananchi wa Brazil kutambua
tunu msingi na mipaka yake, ili kujenga Jamii inayosimikwa katika haki na udugu, hii
ndiyo Jamii inapaswa kujengeka nchini Brazil. Maaskofu wanasema, maandamano haya miongoni
mwa vijana yanachochewa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya mitandao ya kijamii. Haya
ni matokeo ya matatizo na changamoto ambazo hazikupewa ufumbuzi makini nchini Brazil.
Maandamano na vurugu zinazoendelea kwa sasa nchini Brazil ni matokeo na madhara
ya rushwa na ufisadi uliokomaa ndani ya Jamii; ukosefu wa utawala wa sheria, kiasi
kwamba, wananchi wanaamua kujichukulia sheria mikononi mwao! Ni matokeo ya ukosefu
wa ukweli na uwazi, tunu msingi na kielelezo cha utawala bora. Pamoja na kuunga mkono
wasi wasi wa wananchi kuhusu hatima ya maisha yao, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil
linasema, kamwe haliwezi kuunga mkono maandamano yenye vurugu na uvunjaji wa misingi
ya haki na amani. Kanisa haliungi mkono matumizi ya nguvu dhidi ya vijana na waandamanaji.
Matatizo ya wananchi wa Brazil yanapaswa kushughulikiwa na wote, kila mtu
akitekeleza wajibu na dhamana yake bila ya kutegea hata kidogo. Ni jukumu la kila
raia kufuata sheria za nchi, mafao ya wengi, haki na amani na kwamba, kilio cha wananchi
pia kinapaswa kusikilizwa na kamwe wasipuuzwe!