2013-06-24 10:22:38

Mchakato wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa unajikita katika dhana ya upatanisho, haki na amani


Umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa nchini Rwanda ni mchakato endelevu ambao utachukua muda mrefu ili kuweza kukamilika na hivyo kuotesha mizizi yake katika mioyo na maisha ya watu. Ni mchakato ambao hauna budi kujikita katika dhana ya upatanisho, haki na amani.

Haya ndiyo yaliyojitokeza hivi karibuni Jimboni Butare, wakati Wajumbe wa Tume ya Haki na Upatanisho wa Kitaifa iliyoundwa nchini Rwanda, mara tu baada ya mauaji ya kimbari yaliyotokea kunako mwaka 1994 walipotembea Jimboni humo na kuzungumza na viongozi wa Kanisa, waliowakilishwa na Askofu Philippe Rukamba wa Jimbo Katoliki la Butare. Tume ya haki na upatanisho wa kitaifa iliongozwa na Dr. Jean Baptiste Habyarimana, Katibu mkuu wa Tume.

Askofu Rukamba anasema, Tume ina dhamana nyeti itakayosaidia kuibua nguzo msingi zitakazotumika katika ujenzi wa taifa la Rwanda, mahali ambapo, wananchi wake wanaishi kwa kuheshimiana na kuthaminiana; wakiongozwa na kumbu kumbu hai ya historia ya maisha yao, akili na utashi kamili. Haya ni mambo ambayo yanakaziwa pia na Tume ya haki na amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda katika mchakato wa ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa. Ni mambo msingi yanayoweza kuimarisha ujenzi wa nchi kama anavyofafanua Mtakatifu Agostino, Askofu na mwalim wa Kanisa.

Dr. Habyarimana kwa upande wake anasema, Serikali na Kanisa vina dhamana na jukumu la ujenzi wa Rwanda mpya inayosimikwa katika msingi wa haki, amani na upatanisho wa kweli. Hii ni changamoto ya kuunganisha nguvu zao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Wanyarwanda wote. Wajumbe kwa pamoja wameliomba Kanisa kuendeleza Mafundisho yake Jamii na kwamba, Serikali ina wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao bila kusahau uhuru wa kujieleza, kama sehemu ya utekelezaji wa demokrasia makini.








All the contents on this site are copyrighted ©.