2013-06-24 08:04:25

Kuna umati mkubwa wa Wakristo wanaoendelea kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kuliko hata ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo!


Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili ya Kristo ndiye atakayeisalimisha. Huu ni muhtsari wa ujumbe wa Yesu kwa wafuasi wake wa nyakati zote. Mtu kuiangamiza nafsi yake kwa ajili ya Yesu kuna maana kuu mbili: kuiungamana imani au kusimama kidete kutetea ukweli!

Mashahidi na waungama imani ni wale ambao wameyamimina maisha yao kwa ajili ya Yesu Kristo. Katika kipindi cha miaka elfu mbili ya Ukristo kuna Wakristo wengi waliopoteza maisha yao ikilinganishwa na idadi ya Wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Ni mashahidi waliothubutu kujitoa kimasomaso ili kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Hii ni sehemu ya tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya kumi na mbili ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, iliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 23 Juni 2013. Baba Mtakatifu ameendelea kuelezea pia kuhusu mashahidi wa Injili wanaojionesha kila siku ya maisha, wakati wakitekeleza dhamana na wajibu wao kwa Kanisa, Familia na Jamii inayowazunguka.

Hawa ni Makleri, Watawa, Wazazi na Walezi pamoja na vijana. Ni watu wanaoonesha sadaka ya maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake; wanajitahidi kurithisha imani na mafao kwa watoto wao ni vijana wanaojitoa kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji zaidi. Baba Mtakatifu anasema, hata hawa ni mashahidi wa Kristo katika uhalisia wa maisha ya kila siku.

Kuna Wakristo na watu wengine katika Jamii ambao wameyamimina maisha yao kwa ajili ya kulinda na kutetea ukweli, kwani Kristo mwenyewe amesema, Yeye ndiye ukweli na uzima. Kwa mantiki hii, Baba Mtakatifu amekumbuka kwa namna ya pekee, Siku kuu ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu akawaandaa watu kwa ujio wa Kristo na kumwonesha kwao wakati uliopowadia, kama Masiha wa Bwana.

Ndiye Mwana Kondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia. Yohane Mbatizaji, ambaye kwa hakika alikuwa ni zawadi ya Mungu kwa watu wake, alikatwa kichwa kwa kutetea ukweli! Huyu ni kielelezo cha watu wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kulinda na kutetea ukweli, huku wakiongozwa na dhamiri nyofu, ambazo kimsingi ni sheria ya Mungu ilioandikwa katika moyo wa binadamu. Ni watu waliokuwa na msimamo katika maisha, changamoto kwa vijana kuwa na msimamo thabiti na kamwe wasiwe ni bendera kufuata upepo!

Baba Mtakatifu aliwaomba waamini na watu wenye mapenzi mema, kumwomba Bikira Maria ili awasaidie kumwilisha ujumbe wa Injili katika uhalisia wa maisha yao. Huyu ni Mama aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya maisha ya Yesu, hata akadiriki kusimama chini ya Msalaba, akafanikiwa kuuona utimilifu wa mwanga wa ufufuko wa Mwanaye Yesu Kristo. Mwishoni, aliwatakia wote neema na baraka; na akaendelea kuwaomba ili waweze kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala!







All the contents on this site are copyrighted ©.