2013-06-24 15:06:37

Dr. Josephat Muscat akutana na kuzungumza na Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 24 Juni 2013 amekutana na kuzungumza na Dr. Joseph Muscat, Waziri mkuu wa Malta, ambaye pia alikutana na Kardinali Tarcisio Bertone pamoja na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu na mgeni wake, wamezungumzia kuhusu uhusiano kati ya nchi hizi mbili na mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya Malta. Wamekumbushia hija za kichungaji zilizofanywa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita nchini Malta; hizi ni hija ambazo zimeacha kumbu kumbu ya kudumu katika maisha na utume wa Kanisa nchini humo.

Viongozi hawa wamekubaliana kimsingi kwamba, kuna haja ya kuendeleza tunu msingi za maisha ya Kikristo. Wamepongeza mikataba ya uhusiano ambayo imekuwepo kati ya Vatican na Malta hasa katika sekta ya elimu, afya pamoja na utoaji wa elimu shuleni. Angalisho limetolewa kuhusu masuala ya ndoa, mada ambayo itajadiliwa tena kwa wakati muafaka baina ya pande hizi mbili.

Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake wamegusia pia masuala ya kimataifa hususan kwenye Ukanda wa Mediterania, mchango wa Malta katika Umoja wa Ulaya pamoja na mchango makini unaoendelea kutolewa na Malta pamoja na Kanisa kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi.







All the contents on this site are copyrighted ©.