2013-06-24 11:01:36

Boresheni huduma yenu kwa njia ya Sala, Tafakari ya Kina ya Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki na fanyeni yote kwa moyo mkuu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, iliyopita, tarehe 23 Juni 2013 amekutana na kuzungumza na wanachama wa Chama cha Kitume cha Watakatifu Petro na Paulo. Amewashukuru kwa moyo wa ukarimu na majitoleo yao katika huduma kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican wakati wa Maadhimisho ya Ibada na Liturujia mbali mbali za Kanisa.

Huu ni utume unaotekelezwa kama sehemu ya matendo ya huruma na utamaduni kwa kujielekeza zaidi kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii pamoja na kuendelea kutoa majiundo makini kwa vijana wanaotaka kujiunga na Chama hiki, ili waendelee kukua na kukomaa katika kuufahamu upendo na huruma ya Mungu ili waweze kuwaonjesha wale wote wanaokutana nao!

Baba Mtakatifu amewapongeza wanachama wapya ishirini na wawili waliokula kiapo chao ili kwamba, upendo wa Kristo uweze kuwaongoza ili waweze kuwa kweli ni mashahidi wakarimu na wenye uhakika wa kile wanachotenda! Chama hiki ni ushuhuda amini wa maisha ya Kikristo unaowasukuma kujitoa kikamilifu kwa ajili ya huduma kwa jirani na Kanisa katika ujumla wake bila kutarajia ujira, huku wakiendelea kuiga mfano wa Kristo mwenyewe.

Baba Mtakatifu amewaambia Wanachama wa Chama cha Watakatifu Petro na Paulo kwamba, mshahara wao ni furaha ya huduma kwa Kristo na Kanisa lake. Wanachama hawa wanaalikwa kwa namna ya pekee, waboreshe huduma hii kwa njia ya maisha ya Sala, tafakari ya Kina ya Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na kwamba, watekeleze utume wao kwa moyo mkuu. Kwa njia hii ushuhuda wao utakuwa ni wenye mvuto na mguso; huduma kwa watu itaboreka na kuwakirimia furaha zaidi.

Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwatakia kheri na baraka wao pamoja na familia zao! Amewataka hata wao kuwakumbuka na kuwaombea hata wale wanaodhani kwamba ni maadui wao, ili nao pia waonje baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.