2013-06-22 11:03:03

Watoto kutoka katika familia za wakimbizi wanapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kusaidiwa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza linasema kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2013 yamekuwa ni fursa nyingine kwa Jumuiya ya Kimataifa kuweza kufahamu hali halisi inayoendelea katika maisha ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi wanaoteseka kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza linaitaka Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuhakikisha kwamba, inatoa kipaumbele cha kwanza kwa: ulinzi, ustawi na maendeleo ya watoto inapokuwa ikishughulikia masuala ya wahamiaji. Uingereza ni kati ya nchi ambazo zimetia sahihi kwenye itifaki ya kulinda na kutetea haki msingi za watoto, kumbe, inapaswa kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi mkubwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza linaunga mkono taarifa ya pamoja iliyotolewa na Tume ya haki msingi za binadamu kuhusu watoto waliotelekezwa na wazazi wao nchini Uingereza. Taarifa hii inaonekana kwamba, inatoa kipaumbele cha kwanza kwa masilahi kwa mtoto; kwa kuwalinda, kuwawezesha na kuwatetea.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza linakumbusha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya wakimbizi Duniani kwa mwaka 2013, ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa Familia za wakimbizi na wahamiaji, zinazoishi katika mazingira magumu.

Hawa ni watu ambao wakati mwingine wanalazimika kuyakimbia makazi yao, kiasi cha kukosa: amani, ulinzi na usalama. Ni familia ambazo zinakumbana na nyanyaso ya kidini, kisiasa na kijamii. Ni familia ambazo wakati mwingine zinapokelewa kwa macho ya makengeza kutokana na utofauti wa mambo mengi.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, kamwe waamini hawawezi kukaa kitako wakati ambapo ndugu zao wanateseka kama wakimbizi. Familia hizi anasema Baba Mtaklatifu zinapaswa kupendwa, kusaidiwa, kueleweka pamoja na kuonjeshwa ukatimu, kwani wao wanaonesha ile sura ya Kristo Msulubiwa. Mwaliko huu ni muhimu sana kwa Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, wakimbizi wanayo nafasi ya pekee nchini Uingereza.







All the contents on this site are copyrighted ©.