2013-06-22 07:13:11

Wakimbizi wanaopoteza maisha baharini si habari tena!


Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum anasema, tangu mwaka 1988 inakadiriwa kwamba, zaidi ya watu 19,000 wamekufa maji wakati wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kwenda Barani Ulaya kutafuta hali bora zaidi ya maisha.

Hawa ni wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzihama nchi zao kutokana na maafa asilia, vita na magonjwa. Ni watu wanaotafuta usalama wa maisha, kiasi kwamba, wanalazimika kukabiliana uso kwa uso na hatari ya maisha!

Mateso, mahangaiko na hata vifo vya watu hawa si tena habari kwa vyombo vingi vya habari kimataifa, vifo vyao limekuwa eti sasa ni jambo la kawaida halina mashiko wala mvuto! Wadau hawa wanasahau kwamba, hao wanaofariki dunia huko baharini ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kardinali Vegliò ameyasema hayo wakati wa kesha la kuwakumbuka na kuwaombea watu waliofariki dunia wakijitahidi kuvuka bahari ya Meditarania, ili kutafuta malisho ya kijani kibichi. Ibada hii iliyokuwa imeandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio na wadau wengine wanaowahudumia wakimbizi na wahamiaji imefanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria in Trastevere.

Kardinali Vegliò anakumbusha kwamba, nyuma ya idadi ya watu wanaotajwa kuna kundi kubwa la familia, mateso na mahangaiko yao ya ndani, bila kusahau ndoto yao ya kuwa na maisha bora zaidi. Hawa ni watu wanaotamani kuona dunia mpya inayosimikwa kwenye mshikamano wa upendo; dunia ambayo walau kila mtu atakuwa na nafasi ya kuweza kushiriki utajiri na rasilimali kwa ajili ya mafao ya wengi. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watu wanahamasishwa kuelewa na kuthamini hali ya wakimbizi na wahamiaji ili mateso na mahangaiko yao yasibezwe bali yashughulikiwe ipasavyo.

Kardinali Antonio Maria Vegliò anakazia kwamba, ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe na wala haina mjadala na kwa waamini hili linakuwa ni jambo la kupewa kipaumbele cha kwanza. Pili, ukarimu na upendo kwa wageni unapaswa kuwa ni utamaduni ambao unamwezesha mwamini kuona ile sura ya Mungu katika maisha na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao!







All the contents on this site are copyrighted ©.