2013-06-22 10:29:57

Hija ya watoto mjini vatican ili kukutana na kuzungumza na Papa Francisko!


Baraza la Kipapa la Utamaduni linaendelea kuwekeza tunu ya majadiliano katika maisha ya watoto kwani linatambua kwamba, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo! Hata katika utoto wao wanalo jambo la kujifunza na kuwashirikisha wengine, ile furaha, imani na matumaini.

Ni kutokana na mwelekeo huu, Baraza la Kipapa la Utamaduni chini ya uongozi wa Kardinali Gianfranco Ravasi, limeaanda tamasha maalum kwa ajili ya watoto kutoka Jimbo kuu la Milano, watakaosafiri kwa Treni hadi mjini Roma siku ya Jumapili na kupokelewa na Baba Mtakatifu Francisko. Kutoka Milano kutakuwa na jumla ya watoto 71 na watu wazima 60; jumla yao wote ni watu 131.

Treni maalum kutoka Milano, itakapofika mjini Bologna, watoto 115 watapanda, wakisindikizwa na watu wazima 50. Treni hii, itakapowasili mjini Firenze, watoto 61 na watu wazima 40 watapanda ndani ya Treni ili kuendelea na safari kuelekea kituo cha Treni cha Mtakatifu Petro, huko mjini Vatican watapokelewa na Mwenyeji wao Baba Mtakatifu Francisko.

Jumla ya watu 397 watasafiri na Treni maalum kutoka Milano hadi mjini Vatican ili kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kukazia umuhimu kwa jamii kuwalinda, kuwatunza na kuwasaidia watoto kukua: kiroho, kimwili na kimaadili. Watoto watakuwa na mkutano wao maalum kuanzia saa 7: 00 Mchana hadi Saa 9:30 Alasiri, watakapopanda tena Treni na kurudi majumbani mwao.







All the contents on this site are copyrighted ©.