Uchaguzi mkuu ambao ulikuwa umepangwa kufanyika nchini Madagascar hapo tarehe 24 Julai
2013, unaonekana "kupigwa dana dana" baada ya Bi Beatrice Atallah, Mwenyekiti wa Tume
ya Uchaguzi kuonesha wasi wasi wake, hali ambayo imezua hasira kubwa kutoka kwa viongozi
wanaogombea Urais nchini humo.
Wagombea uchaguzi wanaitaka Serikali ya mpito
kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu nchini Madagascar unafanyika katika tarehe iliyopangwa
na kamwe hawawezi kukubali kuahirishwa kwa zoezi hili. Sheria inapaswa kuchukua mkondo
wake.
Kati ya wagombea wanaotarajiwa kutoana jasho jembamba ni Rais wa Kipindi
cha Mpito Bwana Andry Rajoelina, aliyeingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi
kwa kuungwa mkono na Vikosi vya ulinzi na usalama nchini Madagascar. Wengine ni Bwana
Didier Ratsiraka na Bibi Lalao Ravalomanana.