"Tumepiga hatua lakini mapambano dhidi ya Ukimwi baado yanaendelea!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Tanzania
imepata mafanikio makubwa katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi lakini bado kazi ya
kukabiliana na janga hilo ni kubwa. “Ni mapambano magumu lakini kuna dalili kama tunashinda
kwa sababu hali ya leo ni tofauti kabisa na hali ilivyokuwa miaka 10 iliyopita,” Rais
Kikwete alisema usiku wa Jumatano, Juni 19, 2013 Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
Rais
Kikwete alikuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wakuu wa zamani wa Afrika ambao
wanaunda taasisi iitwayo Mabingwa wa Kupambana na Ukimwi (AIDS Champions) Marais Wastaafu
Festus Mogae wa Botswana na Benjamin William Mkapa pamoja na Profesa Miriam Were kutoka
Kenya.
Rais Kikwete aliwaambia viongozi hao katika mkutano huo uliofuatiwa
na chakula cha usiku, “Tumepata mafanikio mengi sana lakini mapambano yenyewe bado
kabisa – kwa sababu bado kuna changamoto mbili kubwa – moja ni kuzuia maambukizi mapya
na pili kuhakikisha wote ambao wameathirika wanaendelea kupatiwa dawa za kurefusha
maisha.”
Rais Kikwete alisema kuwa kampeni ya kupima afya zao ili kujua kama
watu wameathirika ama la inakwenda vizuri na kuwa mpaka sasa Watanzania milioni 18
wamepima afya zao tokea Julai 2007 wakati Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete walipopima
afya zao hadharani katika mkutano wa hadhara Mnazi Mmoja, Dar es Salaam. “Imekuwa
ni kampeni yenye mafanikio makubwa. Siku ile ya kwanza tulipima jumla ya watu 11,000
na tokea siku ile mpaka leo kiasi cha Watanzania milioni 18 wamepima, kiasi cha watu
653,000 wanatumia dawa na kwa hakika aibu iliyokuwa inahusishwa na ugonjwa wenyewe
imepungua sana na inaendelea kupungua,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kazi
yetu kubwa pia iliyoanza na ambayo tutaifanya kwa miaka mitano ijayo ni kuzuia maambukizi
kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa akinamana waja wazito na pia kupunguza kabisa
maambukizi mapya kwa watu wazima. Kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
ni shughuli ambayo tunaifanya chini ya programu yetu ya miaka mitano.”
Rais
Mogae alimpongeza Rais Kikwete na Serikali yake kwa mafanikio hayo makubwa katika
kupambana na ugonjwa ambao unakadiriwa kuwa umeteketeza maisha ya Watanzania milioni
mbili tokea ulipoingia nchini mwanzoni mwa miaka ya 1980. “ Kwa hakika sote katika
Afrika tumetoka mbali sana. Tumepoteza watu wengi sana. Tumepoteza vijana wengi mno.
Nakupongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yako kwa kufikia hatua hii,” Rais Mogae alimwambia
Rais Kikwete.
Naye Rais Mkapa alimwomba Rais Kikwete kushauriana na viongozi
wenzake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) juu ya nchi hizo kushirikiana katika
kujenga kiwanda cha kutengeneza dawa za kurefusha maisha kwa waathirika kwa ukimwi.
“Mheshimiwa Rais lingekuwa jambo zuri kama nyinyi viongozi wa Afrika Mashariki mngeangalia
uwezekano wa kujenga kiwanda cha dawa za ukimwi. Hili lingepunguza mzigo wa fedha
wa kupatikana kwa dawa hizo kutoka nje na pia wakati mwingine hatuwezi kuwa na uhakika
kuwa tutaendelea kupata fedha za kutosha za kuagiza dawa hizo huko mbele.”