Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 12 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa
Ninakuleteeni ujumbe wa Neno la Mungu katika Dominika ya 12 ya Mwaka C. Mama Kanisa
ametuwekea Neno litupalo wajibu wa kutambua yakwamba mfuasi wa Bwana si yule anayefahamu
mambo bali yule anayeishi mafundisho ya Bwana, anayejitwika msalaba wake kila siku
na kumfuasa Bwana.
Katika Injili
ya Luka 9:18-24 ambayo tunaitafakari Bwana yuko faragha anasali, na wanafunzi wako
pamoja naye. Katika kusali anawauliza wanafunzi wake, hivi watu wanasema mimi ni nani?
Na ninyi mwasema mimi ni nani? Kwa hakika anawauliza wanafunzi juu ya asili yake,
anataka wanafunzi wake wawe na uhakika wa yule wanayemfuata ni nani na lengo la maisha
yake ni nini!
Swali la kwanza ni kwa ajili ya kutambua watu wanasema nini na
swali la pili anataka sasa kundi la Mitume hawa katika uhalisia wao waweze kutoa jibu
ambalo litakuwa kielelezo cha mwelekeo wa kazi yao ya kichungaji mara wanapomaliza
malezi yao katika seminari ya Kristo.
Mara moja atufundisha kuishi uhalisia
kamili wa mambo, anataka kila mmoja wetu aingie katika mahusiano ya moja kwa moja
naye na wala si katika makutano. Anataka kila mmoja aingie katika mtima wa dhamiri
yake na kuweza kugundua Bwana ni nani. Anapowauliza atatumia kiwakilishi “ninyi” mwasema
mimi ni nani badala ya “wewe”, katika hili pengine anaona mmoja anaweza kuingia katika
woga na hivi Bwana anataka jibu ambalo linasimikwa katika maisha ya Jumuiya, ndiyo
kusema Kanisa.
Baada ya maswali hayo na hasa swali msingi yaani swali la pili
linakuja jibu halisia toka kwa Mtume Petro akisema “wewe ndiye Kristo wa Mungu” na
kisha Bwana anawaonya wasimwambie mtu yeyote. Katika jibu tunatambua kuwa kumbe Bwana
ni mpakwa mafuta wa Bwana atokaye kwa Mungu, kuhani milele anayetuletea zawadi za
kimungu toka mbinguni. Inaonekana pia alama ya ukuu wa Mt. Petro katikati ya kundi
la Mitume.
Mara baada ya jibu la Mitume Bwana atasonga mbele na kutoa sasa
kiini cha mafundisho yake yaani mateso hadi ufufuko wake ambapo sasa kuna madai makubwa
si kumfahamu tu bali sasa kushika msalaba na kumfuata kila siku. Wanafunzi wanaposikia
mateso haya wataogopa na ndiyo maana hapo mwanzoni aliwaambia wasimwambie mtu. Anatangaza
siri ya kimasiha.
Bwana anataka wanafunzi wake wamfuate kikwelikweli kama
ambavyo alivyo waita mwanzoni alisema nifuate na kumfuata ndo huko kunakotupeleka
mpaka msalabani. Katika kumfuata kuna kupoteza maisha lakini ndiko kuna maisha, yaani
maisha kweli maisha ya milele.
Mpendwa mwana wa Mungu maisha yetu katika imani
yanadai kusimama kidete na kufuata njia ya Kalivari pamoja na Kristo. Ni maisha ya
kujitoa sadaka kwa ajili ya Kanisa na kwa ajili ya wote, ni kumwombolezea yule waliyemchoma
na kwa njia ya majitoleo yako basi neema na zawadi mbalimbali za kimungu zinashuka
toka juu.
Ni kujitahidi daima kujenga umoja wa Kanisa ambao tulipewa kwa njia
ya ubatizo kama ambavyo Mtakatifu Paulo anawaambia Wagalatia akisema: kwa njia ya
Ubatizo wote tumefanywa kuwa sawa. Hakuna tena Myahudi wala Myunani na hapana mtumwa
wala mtu huru.
Basi kila mmoja ni mrithi wa ahadi za Mungu alizotuhaidia kwa
njia ya Ibrahimu. Kumbe sasa msalaba wako ni kujenga usalama na amani katika taifa
la Mungu. Nikutakie Dominika njema na tukutane tena Juma lijalo wasaa na wakati kama
huu. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya
C.PP.S