2013-06-20 15:08:39

Hatuwezi kuomba kwa Baba kama tuna maadui kiroho.


Kuomba kwa Baba Yetu wa mbinguni ni lazima mioyo yetu iwe na amani na ndugu zetu. Papa Francisko, alieleza mapema asubuhi wakati wa Ibada ya Misa, aliyoiongoza katika Kikanisa kidogo cha Mtakatifu Marta mjini Vatican. Papa alisisitiza kuwa, tunaamini katika Mungu ambaye ni Baba, na ambaye yupo karibu nasi , si kama ni Mungu wa kufikirika au miungu hewa ya kidunia.

Katika Misa hiyo, Papa aliiongoza akisaidiana na Kardinali Zenon Grocholewski na miongoni mwa wengine walioshiriki ni kundi la washirika wa Usharika kwa Elimu Katoliki na kundi la wafanyakazi wa Makumbusho ya Vatican.

Papa Fransisko alieleza katika homilia yake kwamba, Maombi si uchawi, lakini ni kujiweka kwa uaminifu katika mkono wa Mungu. Papa, ililenga zaidi katika mafundisho ya Yesu kwa wanafunzi wake, kama ilivyoelezwa katika somo la Injili ya Siku hii. Yesu aliwafundisha wanafunzi wake jinsi ya kusali na si kutoa maneno mengi tu na kelele nyingi batili.

Papa alitoa onyo kwa wale wanaofikiria kwamba maombi na sala ni sawa na uchawi akisema, Maombi si uchawi bali ni kuwa tayari kukumbatiwa na Mungu . Hakuna uchawi hata katika sala za uponyaji bali ni majitoleo ya kuzungumza na Mungu na kumwambia yanayo tusibu tukiwa tumejawa na imani kwake. Hivyo fikara za kuona kama maombi ni uchawi hizo ni fikira za kipagani.

Papa alieleza na kurejea jinsi Yesu alivyo wafundisha wanafunzi wake kusali akisema, sala haipaswi kuwa ya maneno mengi na kupayukapayuka, kwa kuwa Yeye anajua kila kitu. Aliongeza neno la kwanza katika sala ni Baba. Baba ni ufunguo wa sala . Ni lazima kumwomba Baba ambaye yote yanatoka kwake na mwenye kujua maisha yetu yote. Na hivyo hatuwezi kumwomba kwa midomo yetu tu lakini maombi yanapaswa kutoka ndani ya moyo safi usiokuwa na kinyongo kwa miwngine kwa kuwa Yeye nI Mungu wa Upendo.







All the contents on this site are copyrighted ©.