2013-06-19 07:33:58

SADC yaomba kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi nchini Zimbabwe!


Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, wameiomba Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Zimbabwe kuahirisha uchaguzi mkuu uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 31 Julai 2013 ili kupunguza kinzani ambazo zimejitokeza kati ya Rais Robert Mugabe na Waziri mkuu Bwana Morgan Tsvangirai.

Chama cha Upinzani kinamshutumu Rais Mugabe kwa kutia sahihi waraka wa serikali kuhusu mabadiliko ya uchaguzi, kitendo kinachovunja makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa kuhusu ugawanaji wa madaraka katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. SADC inapendekeza kwamba, uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe ufanyike tarehe 25 Agosti 2013.

Lakini pendekezo hili linapaswa kupelekwa kwenye Mahakama kuu ya Zimbabwe ili iweze kutoa uamuzi wa kisheria. Ni matumaini ya SADC kwamba, uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe hautakuwa tena chanzo cha migogoro na kinzani nchini Zimbabwe.

Wachunguzi wa mambo wanasema, pengine shutuma hizi hazina msingi, ikiwa kama Serikali ya Kitaifa ilikuwa na muda wa miaka minne na nusu kuweza kufanya mabadiliko katika sheria za uchaguzi na haikuweza kufanikisha yale yaliyokuwa yanakusudiwa, itawezekanaje kuharakisha masuala haya katika kipindi cha mwezi mmoja tu?








All the contents on this site are copyrighted ©.