Monsinyo Battista Ricca ateuliwa kuwa Katibu mkuu wa Tume ya Makardinali inayosimamia
na kuratibu Benki ya Vatican
Tume ya Makardinali inayosimamia na kuratibu shughuli za Benki ya Vatican IOR imemteua
Monsinyo Battista Mario Salvatore Ricca kuwa katibu mkuu wa Tume ya Makardinali inayosimamia
Benki ya Vatican na uteuzi huu kuridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, atahudhuria
mikutano ya Taasisi hii ya fedha ya Vatican kadiri ya sheria na kanuni za IOR. Hayo
yamefafanuliwa na Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican hivi karibuni.
Monsinyo
Battista Ricca ni kati ya viongozi waandamizi wa huduma ya kidiplomasia mjini Vatican
pia ni mkurugenzi mkuu wa Nyumba za Mapadre zinazomilikiwa na kuendeshwa na Vatican.
Monsinyo Ricca anachukua nafasi ya Askofu mkuu Pierro Pioppo aliyeteuliwa hivi karibuni
kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Cameroon na Equatorial Guinea. Yeye alikuwa ni Katibu
wa Tume ya Makardinali kwa ajili ya Benki ya Vatican kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka
2010.
Kwa uteuzi wa Bwana Ernst Von Freyberg kuwa Rais wa Benki ya Vatican
na sasa uteuzi wa Monsinyo Battista ricca, Tume ya Makardinali imeziba mwanya wa uongozi
wa Benki ya Vatican; nafasi ambayo ilikuwa wazi kwa muda kadhaa.