Maadhimisho ya Mkutano wa Wakuu wa G8 ilikuwa ni fursa nyingine iliyotumiwa na Makanisa
nchini Uingereza kuwakumbusha wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, baa la njaa ni
mapambano shirikishi yanayopaswa kuanza kutimua vumbi kwenye mizizi ya tatizo ili
mamillioni ya watu wasiendelee kuteseka duniani kwa kukosa chakula.
Makanisa
nchini Uingereza hivi karibuni yalizundua Kampeni iliyoongozwa na kauli mbiu “Chakula
cha kutosha kwa kila mtu”. Ili kuwakumbusha viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa
kwamba, baa la njaa si mchezo, kwani kuna mamillioni ya watu wanaendelea kupotza maisha
yao na kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto ambao wamekumbwa na utapiamlo wa kutisha.
Hakuna sababu msingi wanasema viongozi wa Makanisa nchini Uingereza dunia
kuzalisha chakula cha kutosha na baadhi ya watu duniani wakaendelea kuteseka kutokana
a baa la njaa na utapiamlo! Waamini kutoka Madhehebu mbali mbali ya Kikristo walikusanyika
hivi karibuni kusali na kufunga kama kielelezo cha mshikamano wao wote wanaoteseka
na baa la njaa duniani, mfumo unaoendelea kuwanufaisha watu wenye nguvu kiuchumi na
kisiasa.
Huu ni mwelekeo wa kukosekana kwa misingi ya haki duniani. Baadhi
ya viongozi wa Kanisa wanasema kuna wanasiasa nchini humo wameshindwa kuweka moyo
wa ”nyama” katika mikakati na vipaumbele vyao kisiasa kwani wanaelemewa mno na masilahi
binafsi.
Askofu Mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury ambaye pian i Kiongozi
mkuu wa Kanisa Anglikani Duniani, ametumia fursa ya mkutano huu kumshukuru na kumpongeza
Waziri mkuu David Cameron ambaye ameahidi kwamba, Uingereza itatenga kiasi cha asilimia
0.7% cha Bajeti yake kwa ajili ya misaada ya kimataifa kila mwaka.
Anakumbusha
kwamba, G8 ni kundi kubwa lenye uwezo: kifedha na kiuchumi, likipania na kutekeleza
ahadi zake kwa vitendo, maendeleo makubwa yanaweza kupatikana. Hata katika nyakati
za athari za myumbo wa uchumi kimataifa, bado waamini na wananchi wenye mapenzi mema
wanachangamotishwa na Kanisa kujenga na kuimarisha mshikamano wa dhati unaoongozwa
na Kanuni Auni, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Ni matumaini
ya Askofu mkuu Justin Welby kwamba, wakuu wa G8 katika mkutano wao unaohitimishwa
tarehe 18 Juni 2013 wataweza kuibua mbinu mkakati wa mshikamano na nchi changa zaidi
duniani. Waziri mkuu David Cameron anasema kwamba, wameisikia Kampeni ya viongozi
wa kidini dhidi ya baa la njaa na wataendelea kulifanyia kazi wazo hili. Mwaka 2013
uwe ni mwanzo wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani.