2013-06-17 08:33:14

“Kuondoa Mila Zenye Kuleta Madhara kwa Watoto: Ni Jukumu Letu Sote”


Ifuatayo ni hotuba ya Mheshimiwa Sophia M. Simba, Waziri maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto nchini Tanzania alipokutana na waandhisi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofikia kilele chake tarehe 16 Juni 2013.


Ndugu Waandishi wa Habari,

Tarehe 16 Juni, 2013 ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika. Siku hii huadhimishwa na nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika kwa mujibu wa Azimio lililopitishwa na nchi 51 za Umoja huo mwaka 1990. Azimio hili lilipitishwa kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya watoto wa shule yaliyofanyika katika kitongoji cha Soweto, Afrika ya Kusini tarehe 16 Juni 1976. Kama tunavyofahamu siku kama hiyo watoto wapatao 2,000 waliuwawa kikatili na iliyokuwa Serikali ya Makaburu wakati wakiwa kwenye harakati za kudai haki yao ya msingi ya kutokubaguliwa kutokana na rangi yao. Kwetu sisi Watanzania siku hii ni muhimu sana kwa vile inazingatia maslahi ya watoto. Inatukumbusha sisi wazazi, walezi, taasisi/mashirika na Serikali kwa ujumla kuhusu wajibu na majukumu yetu kwa watoto.

Lengo na madhumuni:

Tanzania kama mwanachama wa Umoja wa Afrika, imekuwa ikishiriki kikamilifu kuadhimisha siku hii kwa miaka ishirini na mbili mfululizo tangu mwaka 1991. Lengo la maadhimisho haya ni kuelimisha wananchi kuhusu haki, ustawi na maendeleo ya watoto wa jinsi zote. Kwa upande wao, watoto wanapata nafasi maalum ya kujieleza, kusikilizwa, kushiriki na kuonyesha vipaji vyao katika hatua za kujiendeleza wakati wa maadhimisho haya. Kwa ujumla madhumuni ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ni pamoja na:-

·Kuinua kiwango cha uelewa na ufahamu wa matatizo yanayowakabili watoto wa Afrika
·Kukumbusha na kuhamasisha jamii kuhusu utoaji wa haki za msingi za watoto.
·Kuwaendeleza watoto kielimu, kiafya, kiutamaduni na kimaadili na kuhakikisha ustawi wa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Aidha, Serikali kwa kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto hutumia siku hii:-
·Kutathmini kwa kina utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto, Sera nyingine za kisekta zinazohusu watoto, Sheria ya Mtoto Na.21/2009 pamoja na mikataba ya kimataifa na kikanda kuhusu haki na ustawi wa Mtoto.
·Kuhakikisha watoto wanapata nafasi ya kujieleza na kusikilizwa katika masuala yanayohusu maendeleo na ustawi wao, kwa kupitia fursa tulizo nazo ikiwa ni pamoja na kutumia vyombo vya habari vya taifa.
·Kuhimiza kuwekeza rasilimali za kutosha katika afya, elimu na lishe bora ya watoto kama haki zao za msingi.

Kaulimbiu
Katika kuadhimisha maadhimisho haya tumekuwa na kawaida ya kuandaa kaulimbiu ambayo kwa namna moja ama nyingine inalenga kuihamasisha jamii kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakumba watoto nchini na Afrika kwa ujumla. Mfano kaulimbiu ya mwaka 2011 ilikuwa ni “Tuungane kwa Pamoja Kuchukua Hatua za Haraka Kushughulikia Tatizo la Watoto Wanaoishi Mitaani(All Together for Urgent Actions in Favour of Street Children)”, kaulimbiu ya mwaka 2012 ilikuwa ni “Haki za Watoto Wenye Ulemavu: Ni Wajibu Wetu Kuzilinda, Kuziheshimu, Kuziendeleza na Kuzitimiza (The Rights of Children With Disabilities: The Duty to Protect, Respect,Promote and Fulfill)”.

Hivyo basi, kaulimbiu ya mwaka 2013 inasema “Kuondoa Mila Zenye Kuleta Madhara kwa Watoto: Ni Jukumu Letu Sote” (Eliminating Harmful Social and Cultural Practices: Our Collective Responsibility). Lengo la kaulimbiu hii ni kuihamasisha jamii yetu kubaini baadhi ya mila ambazo zimekuwa zikipelekea madhara mbalimbali kwa watoto wetu iwe ni kimwili na hata kisaikolojia. Kuendelea na mila hizi kunakinzana na utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008), Sheria ya Mtoto Na. 21/ 2009 na mikataba ya kimataifa na kikanda kuhusu haki na ustawi wa watoto ambayo nchi iliiridhia.


Ndugu Waandishi wa Habari
Nchi yetu ina makabila mbalimbali ambapo kila kabila lina mila na tamaduni zake. Mila hizi kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikisaidia kuleta amani na uelewano katika jamii zetu, lakini vile vile mtakubaliana nami kuwa kuna baadhi ya mila zimeleta changamoto kubwa katika kumtimizia mtoto haki zake za msingi. Haki hizi ni pamoja na haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutokubaguliwa.

Naomba nitoe mfano wa tatizo la ukeketaji kwa watoto wa kike linalofanywa na baadhi ya makabila hapa nchini. Kitendo hiki kinakinzana na haki nilizozitaja hapo juu kwa kiasi kikubwa hasa ukichukulia namna zoezi zima la ukeketaji linavyofanyika na mazingira yake ambapo mtoto anawekwa katika mazingira mepesi ya kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi na hatimaye kuathirika na UKIMWI. Lakini pia zoezi hili humuathiri sana mtoto kisaikolojia kutokana na namna linavyoendeshwa. Hivyo basi, pamoja na kutambua umuhimu wa mila zetu hapa nchini, kuna haja sasa ya kuzifanyia tathmini ya mchango wake katika suala la malezi, makuzi na maendeleo ya awali na ya baadaye kwa watoto wetu.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Napenda kuchukua fursa hii pia kuwataarifu kuwa maadhimisho haya kwa mwaka huu yataadhimishwa katika ngazi ya Mkoa ambapo kila mkoa utaaadhimisha siku hii kwa kushirikisha na Halmashauri za wilaya/Manispaa/Miji, kata, vijiji, mashirika na taasisi mbalimbali zilizoko katika Mkoa husika na watu binafsi. Hii itaipa mikoa nafasi nzuri ya kutafakari matatizo yanayowakabili watoto ikiwa ni pamoja na kuwapatia haki zao za msingi. Mikoa itapata pia nafasi ya kuweka miradi endelevu kwa ajili ya kuwandeleza watoto.

Mwisho
Ndugu zangu wanahabari nawashukuru kwa ushirikiano wa hali ya juu kama mnavyofanya mara nyingi katika kuihamasisha jamii yetu kuhusu masuala ya watoto na maendeleo yao. Napenda kuwapongeza na kuwashukuru sana kwa kushirikiana na Wizara yangu katika kuijenga “Tanzania Imfaayo Mtoto”. Ni matumaini yangu pia mtaendelea kuwa chanzo kizuri cha kufichua vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto kama ambavyo mmekuwa mkifanya kwa muda mrefu sasa.

Baada ya kusema haya, naomba niwatakie wananchi wote maadhimisho mema ya siku hii na kila mmoja wetu aangalie ni vipi anashiriki kumpatia mtoto wake na watoto wote wa Tanzania haki zao. Hili ni jukumu letu sote.

Asanteni sana kwa kunisikiliza na nawatakia kazi njema








All the contents on this site are copyrighted ©.