2013-06-17 07:39:27

Waamini wanaalikwa kusherehekea huruma na upendo wa Mungu unaojionesha katika maisha na utume wa Yesu!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, mwishoni mwa juma, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa waamini wa Kanisa Katoliki wanaoishi na kufanya kazi Jijini Dubai, kwenye Falme za Kiarabu, akiwaalika kwa namna ya pekee kusherehekea huruma na upendo wa Mungu unaojionesha katika maisha na utume wa Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ili kumkirimia mwanadamu maisha ya uzima wa milele na kwamba, huruma ya Mungu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko daima inashinda.

Hii ndiyo huruma ya Yesu inayojionesha katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya kumi na moja ya kipindi cha Mwaka wa Kanisa, pale Yesu anapomsamehe na kumwondolea dhambi Maria Magdalena aliyefahamika mtaani kuwa ni mzinzi wa kutupwa! Anajinyenyekesha mbele ya Yesu kwa machozi ya toba, kiasi kwamba, anaonja huruma na upendo unaobubujika kutoka moyoni mwa Yesu ambaye analaani dhambi, lakini anamhurumia na kumkumbatia mdhambi, huku akimwonesha njia mpya ya kufuata, ili aweze kutembea katika mwanga wa Kristo mfufuka!

Kanisa linawahamasisha waamini kuogopa dhambi n anafasi zake, wa kujikita zaidi na zaidi katika upendo wa Mungu kwa njia ya mshikamano wa dhati, kwa ajili ya upendo na huduma kwa Mungu na jirani. Kanisa, anasema Kardinali Filoni linatambua na kukiri dhambi zinazotendwa na watoto wake, changamoto kwa Wakristo kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwasafisha na kuwakirimia tena maisha mapya.

Kuna kundi kubwa la wanawake wanaosimuliwa katika Agano Jipya waliotumia karama na vipaji vyao kwa ajili ya kumhudumia Yesu Kristo katika maisha na utume wake; changamoto na mwaliko kwa waamini kuwawezesha wachungaji wao ili waweze kutekeleza utume wao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kutambua kwamba, kila mwamini amejaliwa karama na utajiri anaoweza kuwashirikisha jirani zake, ili kujenga na kuliimarisha Kanisa.

Kardinali Filoni anawataka waamini katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kuendelea kutolea ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake; wakitambua kwamba, wao pia ni wadau wa dhamana ya Uinjilishaji Mpya unaopaswa kuanzia ndani ya familia, maeneo ya kazi na katika medani mbali mbali za maisha, ili majirani wao waweze kuonja ile furaha ya Injili.








All the contents on this site are copyrighted ©.