2013-06-17 07:48:30

Ujumbe wa Maaskofu kwa wakuu wa G8


Maaskofu wa Makanisa mbali mbali duniani wamewaandikia barua ya wazi wakuu wa G8 wanaokutana katika mkutano wao wa mwaka kuanzia tarehe 17 hadi 18 Juni 2013 huko Enniskillen, Ireland kuwasihi kuangalia kwa jicho la huruma hatima ya maskini duniani wakati wa majadiliano yao. Maaskofu wanasema, ustawi na maendeleo ya nchi yanapimwa kutokana na mikakati na sera za serikali katika kuwajali wanyonge na maskini ndani ya jamii husika. RealAudioMP3

Maaskofu wanasema, umefika wakati kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kupambana na baa la umaskini, njaa na ujinga vinavyoendelea kumwandama mwanadamu katika maisha yake hapa duniani licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali vitu, fedha, watu na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hii ni changamoto endelevu inayotolewa pia na Baba Mtakatifu Francisko katika utume wake ndani ya Kanisa kwa sasa.

Kuna haja ya kuwawezesha wakulima wadogo wadogo wanaoishi kwenye nchi changa zaidi duniani ili waweze kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya chakula, utunzaji na ugavi ili hatimaye, dunia iweze kuondokana na baa la njaa na utapiamlo unaowaandama mamillioni ya watu duniani.

Maaskofu wanawataka wakuu wa G8 kulivalia njuga tatizo la ukwepaji kodi unaofanywa na baadhi ya watu wenye “vijisenti vyao”, kwani hii ni dhamana ya kiraia na kimaadili kwa kila mwananchi kama njia ya kuchangia mafao ya wengi, mchango ambao utaisaidia maboresho ya huduma mbali mbali za kijamii. Maaskofu wanasema pia kwamba, kuna haja ya kuwa na sera makini katika soko la dunia kwa kuondokana na ukiritimba ambao umesababisha mkwamo wa uchumi kwa nchi changa zaidi duniani kutokana na uwepo wa mashindano yasiyokuwa na uwiano sawa.

Nchi changa zimejikuta zikiwa ni walaji wakuu wa mazao na bidhaa zinazozalishwa kwenye nchi tajiri zaidi duniani, hali ambayo inakwamisha maendeleo kwa wakulima kutoka katika nchi changa zaidi duniani. Maaskofu wanakumbusha pia ujumbe wa Baba Mtakatifu Franciko kuhusu matumizi bora ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya mafao ya wengi na katika kudumisha na kuendeleza mchakato wa kutafuta: haki, amani na maendeleo endelevu ya binadamu yanayogusa mahitaji yake msingi.

Ni matumaini ya Maaskofu wa Makanisa kwamba, utajiri na rasilimali nyingi inayopatikana katika nchi changa zaidi duniani badala ya kuwa ni laana na chanzo cha kinzani, migogoro na vita, itageuka kuwa ni baraka na neema kwa wananchi wake.

Wakati huo huo, Askofu mkuu Justin Portal Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani anatarajia kuzindua kampeni ya kimataifa dhidi ya baa la njaa duniani; kampeni inayoongozwa na kauli mbiu “Chakula kwa wote”. Kampeni hii inayashirikisha mashirika ya misaada kimataifa na watawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaotaka wakuu wa G8 kujifunga kibwebwe kupambana kufa na kupona na baa la njaa duniani linaloendelea kudhohofisha utu na maisha ya watu wengi duniani.

Kwa kuonesha nia hii njema, hivi karibuni, Maaskofu walifanya mfungo wa kujinyima chakula, tukio ambalo liliungwa mkono na maelfu ya waamini ili kuonesha uchungu wa baa la njaa duniani. Dunia ina uwezo wa kuzalisha chakula kwa kila mtu, lakini jambo la kusikitishani kuona kwamba, si watu wote wanapata chakula cha kutosha. Maaskofu pia wanawataka wakuu wa G8 kutekeleza ahadi zao kwa vitendo katika kuchangia mchakato wa maendeleo endelevu kwa ajili ya chi changa duniani.








All the contents on this site are copyrighted ©.