Wajumbe wa Vietnam na Vatican waliridhishwa na mchakato wa uhusiano kati ya nchi hizi
mbili!
Mkutano wa nne wa kikosi kazi cha ushirikiano kati ya Vatican na Vietnam umehitimishwa
hivi karibuni mjini Vatican. Ujumbe wa Vietnam kwenye mkutano huu uliongozwa na Bwana
Bui Thanh Son, Naibu Waziri wa mambo ya nchi za nje na ujumbe wa Vatican uliongozwa
na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican.
Wajumbe pamoja na mambo mengine wamepembua uhusiano
kati ya Vatican na Vietnam pamoja na Kanisa Katoliki nchini humo katika ujumla wake.
Vatican imeishauri Serikali ya Vietnam kuendelea kuboresha uhuru wa kuabudu pamoja
na kutoa nafasi kwa dini kuchangia ustawi na maendeleo ya nchi yao kiuchumi na kijamii.
Vatican imeishukuru Serikali ya Vietnam kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha
Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Asia uliofanyika nchini humo kunako Mwezi Desemba 2012.
Vatican pia imeishukuru
Serikali kwa ushirikiano mwema wakati wa ziara ya kikazi iliyofanywa na Askofu mkuu
Leopoldo Girelli nchini humo na kwamba, imeonesha utashi wa kuanzisha uhusiano wa
kidiplomasia na Vietnam kwa kuwa na mwakilishi wa Vatican nchini humo kwa ajili ya
mafao ya pande hizi mbili.
Ujumbe wa Vatican umesema kwamba, Kanisa litaendelea
kuchangia kwa hali na mali ustawi na maendeleo ya nchi ya Vietnam, kwa kumwilisha
Injili sanjari na waamini wake kuendelea kuwa ni raia wema. Kanisa litaendelea pia
kutoa Mafundisho yake Jamii kwa wananchi wa Vietnam.
Pande hizi mbili zinaridhishwa
na uhusiano ambao umekuwepo kati yao, kwa kuendelea kushirikiana vyema pamoja na kubadilishana
misingi ya uhusiano wa kidiplomasia na kwamba, wataendelea kujenga uhusiano zaidi
kwa kuwezesha kuwa na Balozi wa Vatican nchini Vietnam asiyemkazi, ili kumwezesha
kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu zaidi.
Mkutano wa awamu ya tano unatarajiwa
kufanyika mjini Ha Noi, nchini Vietnam na kwamba, mkutano huu utapangwa kufuatia mazungumzo
ya kidiplomasia. Wajumbe kutoka Vatican walipata nafasi ya kukutana na kuzungumza
na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa Kimataifa mjini Vatican.