2013-06-15 14:23:01

Waamini wanachangamotishwa kuwa ni wadau wa huduma ya mapendo kwa jirani zao kama njia ya kukoleza misingi ya amani!


Kanisa Katoliki linaendelea kushirikiana na waamini wa dini mbali mbali kwa ajili ya kuombea na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kwa ajili ya mafao ya wengi na ustawi wa binadamu mahali popote pale alipo. Huduma na amani ni chanda na pete katika maisha ya waamini. Ni changamoto iliyotolewa na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini wakati wa sala ya pamoja kwa ajili ya kuombea amani iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Kanisa kuu la Westminster, Jumamosi tarehe 15 Juni 2013.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Tauran yuko nchini Uingereza kwa ziara maalum ya kikazi inayopania pamoja na mambo mengine kujenga na kuimarisha urafiki urafiki miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali ili kwa pamoja waweze kusimama kidete kulinda na kutetea amani, changamoto kutoka kwa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, ambayo inaendelea kufanyiwa kazi kwa sasa.

Umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali ni nyenzo msingi katika kujenga na kudumisha amani. Katika ziara yake nchini Uingereza, Kardinali Tauran amekutana na waamini wa dini ya Kihindu, Kijanisti na siku ya Jumamosi, amekutana na waamini wa dini la Kisikh, wanaohamasishwa kushirikiana ili kujenga misingi ya haki na amani. Ni mwaliko kwa waamini wa dini hizi mbili kufahamu kwamba, kuna furaha kubwa kwa waamini kutolea muda, vipaji, karama na nguvu zao kwa ajili ya mafao na furaha ya wengine.

Kardinali Tauran anasema kwamba, ulimwengu mamboleo umesheheni tabia ya watu kutaka kumezwa zaidi na malimwengu, hali inayoonesha ulaji wa kutupwa, mmong'onyoko wa kimaadili na utu wema; ubinafsi, tamaa na uchu wa mali na madaraka; mambo ambayo kwa namna moja au nyingine yanachangia kinzani na migogoro ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na pengo kubwa kati ya maskini na matajiri; na umati wa watu unaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Waamini wanaweza kuchangia katika mchakato wa kuleta ugawanaji sawa wa rasilimali, mapato na utajrii wa nchi pamoja na fursa mbali mbali zinazojitokeza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi husika. Kwa pamoja wasimame kidete kupinga vitendo vya rushwa, wizi, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma; daima wakijitahidi kujenga na kudumisha Jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na usawa kwa ajili ya mafao ya wengi.

Kardinali Tauran anasema kwamba, kuna uhusiano mkubwa wa uelewa wa huduma kama kielelezo cha upendo kwa Mungu na jirani, hali inayojionesha kwa namna ya pekee kutoka kwa Kristo aliyewaambia mitume wake kwamba, hakuja ulimwenguni ili kuhudumiwa bali kuhudumia na kutoa maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi.

Waamini wa dini hizi mbili wanaweza kutolea ushuhuda kama mtu binafasi au kama Jumuiya kwa njia ya huduma inayomwilishwa katika matendo. Huduma hii itolewe kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa njia ya majadiliano ya kidini na ujenzi wa amani, daima wakijitahidi kuendeleza mchakato wa kutafuta ukweli na amani ya kudumu.







All the contents on this site are copyrighted ©.