Tafuteni mafao ya wengi; dumisheni utu na heshima ya binadamu!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 15 Juni 2013 amekutana na kuzungumza na
Wabunge kutoka Ufaransa wanaowakilisha sera na maoni tofauti, lakini kwa pamoja wameonesha
uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Ufaransa. Anasema, anapenda kukazia dhamana
na wajibu walio nao wabunge na Kanisa katika maisha ya hadhara.
Baba Mtakatifu
anatambua kwamba, Serikali ya Ufaransa haina dini na kwamba, uhusiano wake na dini
pamoja na madhehebu mbali mbali nchini humo hauna haja ya kuwa na misigano inayopelekea
hata dini na mashirika yake kutohusishwa kikamilifu katika ujenzi, ustawi na maendeleo
ya wananchi wa Ufaransa. Kwa pamoja wanaweza kusimama kidete kulinda na kudumisha
utu na heshima ya binadamu pamoja na kutafuta mafao ya wengi mambo ambayo ni sehemu
ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kanisa linapenda kuchangia katika ustawi na maendeleo
ya wananchi wa Ufaransa katika medani mbali mbali za maisha.
Kama wawakilishi
wa wananchi waliowachagua katika ngazi ya kitaifa, Wabunge wanahamasishwa kushiriki
kikamilifu katika maboresho ya maisha ya wapiga kura wao kwa kuguswa na mahitaji yao
msingi. Kama wabunge, wanatekeleza majukumu yao mintarafu sheria ambazo zinapaswa
pia kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya mwanadamu.
Baba Mtakatifu
Francisko, mwishoni anawatakia kila la kheri na baraka tele katika utume wao kwa wananchi
wa Ufaransa, daima wakitafuta mafao ya wengi sanjari na kudumisha umoja na udugu miongoni
mwao!