2013-06-15 10:57:38

Kuchelewesha mchakato wa kuandika Katiba Zambia kunaonesha harufu ya ufisadi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia linaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, mchakato wa kuandika Katiba Mpya nchini humo utawasaidia wananchi wa Zambia kuwa na Sheria Mama itakayokuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao katika medani mbali mbali. Wanahitaji katiba itakayowawezesha wananchi wa Zambia kupata huduma bora za kijamii.

Ili kufanikisha mchakato huu kuna haja kwa Serikali kuhakikisha kwamba, mchakato unafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na vipaumbele vya nchi, ili kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Zambia ambao wengi wao kwa sasa wanaogelea katika dimbwi la umaskini, ujinga na maradhi.

Hayo yamesemwa na Padre Cleophas Lungu, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia wakati akichangia maoni kwenye mkutano uliokuwa unaratibu maoni ya maboresho ya muswada wa Katiba ya Zambia ambayo watu wengi wanasema kwamba, imechukua muda mrefu kuandikwa na kila wakati wajumbe wa Tume ya kurekebisha Katiba wanaomba kuongezewa muda ili kuratibu maoni ya wananchi, jambo ambalo wananchi wa Zambia wanasema, kuna harufu ya rushwa na ufisadi!

Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia linawaalika waamini na wananchi kwa ujumla wao kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maboresho ya muswada wa Katiba na kwamba, hili si jukumu la wanasiasa peke yao. Tangu mwaka 1964 Zambia ilipojitwalia uhuru wake kutoka kwa Mwingereza, imekwishafanya mabadiliko ya Katiba mara nne.







All the contents on this site are copyrighted ©.