2013-06-15 08:20:21

Kanisa kwa heshima ya Mtakatifu Anthoni wa Padua latabarukiwa Dubai, Falme za Kiarabu!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Ijumaa tarehe 14 Juni 2013, akiwa nje kidogo ya Jiji la Dubai, Falme za Kiarabu, ametabaruku Kanisa kwa heshima ya Mtakatifu Anthoni wa Padua katika kitongoji cha Ras Al khaimah. Ni Kanisa lililojengwa kwa upendo na mshikamano kati ya Familia ya Mungu nchini Falme za Kiarabu inayoundwa na Waamini wa Kanisa Katoliki wapatao millioni 2. 5 kutoka katika Mataifa 90.

Katika mahubiri yake, Kardinali Filoni amewakumbusha waamini hao kwamba, wao ni Hekalu hai la Mungu, ambao wameshikamana ili kujenga Kanisa kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ndiye mjenzi mkuu wa Kanisa lake na kwamba, kila mmoja wao ni jiwe muhimu sana katika kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa. Itakumbukwa kwamba, hili ni Kanisa la nane kujengwa na Kanisa Katoliki katika Falme za Kiarabu na kwamba, hili ni tukio muhimu sana wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani.

Kardinali Filoni amewapatia salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, amewashukuru viongozi wa Serikali kwa moyo wa ushirikiano waliouonesha kwa Kanisa Katoliki nchini humo. Hawa ni waamini wanaotoka katika nchi mbali mbali duniani, lakini kwa pamoja wanaunda Familia ya Mungu, huku wakishuhudia utajiri wa tamaduni na umoja katika imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kila mwamini anachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa ni jiwe hai katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, Kristo ndiye jiwe kuu la pembeni na lenye nguvu na uwezo wa kuleta mabadiliko ya kina katika ulimwengu huu.

Kardinali Filoni anawaalika Wakristo kushuhudia imani yao kwa moyo wa furaha matumaini na chachu ya utakatifu wa maisha, miongoni mwa wale wanaowazunguka. Wawe ni mfano na kielelezo cha watu wanaochapa kazi kwa juhudi na maarifa huku familia zao zikiwa ni mfano wa kuigwa katika maisha ya kiroho. Ushuhuda wa maisha yao ujioneshe katika imani, sala za kila siku; huruma na upendo kwa wafanyakazi wenzao na jirani wanaoishi nao! Wawe ni kielelezo cha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na utulivu.

Katika hija ya maisha yao wajitahidi kuwa ni kielelezo cha ushuhuda wa upendo wa Mungu. Mtakatifu Anthoni wa Padua awe ni msimamizi katika safari ya maisha yao huko ugenini. Bikira Maria Mama wa Falme za Kiarabu aliyetangazwa kunako tarehe 16 Januari 2011 awe ni mwombezi wao katika shida na raha.







All the contents on this site are copyrighted ©.