Jeshi la Polisi kushirikiana na viongozi wa Kanisa kupambana na uhalifu ndani ya Jamii
Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, hivi karibuni
alikutana na kuzungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Insipekta Jenerali Said Mwema.
Kardinali Pengo anasema kwamba, viongozi wa dini wanaowajibu mkubwa katika kuhimiza
maadili, utii wa sheria na upunguzaji wa matukio ya uhalifu nchini Tanzania pamoja
na kuhakikisha kwamba, Serikali inatekeleza wajibu wake msingi wa ulinzi na usalama
kwa raia wake.
Viongozi wa Kanisa wanaweza kusaidia mchakato wa kuboresho ya
maadili miongoni mwa jamii kwa njia ya mahubiri na mifano bora ya maisha, jambo ambalo
linaweza kuwa ni msaada mkubwa katika kukabiliana na uhalifu ndani ya Jamii.
Mkuu
wa Jeshi la Polisi kwa upande wake, amesema, umefika wakati kwa Jeshi la Polisi na
Viongozi wa Kanisa kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuhakikisha kwamba, utawala wa
sheria unatekelezwa na kuzingatiwa na kwamba, wavunjaji wa sheria wanafikishwa mbele
ya sheria. Ongezeko la vitendo vya uhalifu ndani ya Jamii ni changamoto kubwa hata
kwa viongozi wa Kanisa, ambao wana wajibu wa kufundisha na kuhimiza maadili na utu
wema.
Mkutano kati ya Kardinali Pengo na Mkuu wa Jeshi la Polisi umehudhuriwa
pia na Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa pamoja na Askofu msaidizi Titus Mdoe wote
kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam.