2013-06-14 14:34:57

Wakristo wanachangamotishwa kuishi na kushirikiana kwa pamoja kama kielelezo cha ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake!


Baba Mtakatifu Francisko amemkaribisha Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani, kwa kutambua kwamba, Yeye si mgeni bali ni sehemu ya "watakatifu na Familia ya Mungu". Anamshukuru kwa kumwombea wakati alipokuwa anaanza utume wake kama Askofu wa Roma na kwamba, ni jambo jema kusindikizana kwa njia ya sala.

Baba Mtakatifu amegusia historia tete ya uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikani na jitihada ambazo Makanisa haya mawili imezitekeleza katika kujenga na kudumisha upendo na udugu, jambo ambalo kwa pamoja wanapenda kumshukuru Mungu.

Ni hija ambayo imeshuhudia kuundwa kwa Tume ya Ushirikiano wa Kimataifa kati ya Makanisa haya mawili ili kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwa kuheshimiana na kuthaminiana katika kudumisha hali ya upendo na urafiki kama inavyojionesha kwa uwepo wa Askofu mkuu Vincent Nichols Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza.

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru viongozi wa Kanisa Anglikani kwa kutambua na kuthamini mawazo na nia iliyopelekea Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kuanzisha Majimbo maalum ili kukidhi hamu ya Waamini wa Kanisa Anglikani waliotaka kwa hiyari yao wenyewe kujiunga na Kanisa Katoliki. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini hao wataweza kushirikisha tasaufi, liturujia na mapokeo ya kichungaji kutoka katika Kanisa Anglikani na hivyo kumwilisha amana hii kwa Kanisa Katoliki.

Mkutano wa viongozi hawa wawili anasema Baba Mtakatifu Francisko ni kuwakumbusha kwamba, wanayo dhamana ya kutafuta umoja miongoni mwa Wakristo kama sehemu ya utekelezaji wa utashi wa Kristo mwenyewe aliyewaunganisha pamoja na kuwa kaka na dada na hivyo kuunda Familia ya Baba mmoja na kwamba, sala yao ya pamoja ina umuhimu wa pekee katika hatima hii.

Sala inawawezesha Wakristo kuchuchumalia umoja unaopaswa kujionesha katika medani mbali mbali za maisha, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo kama vile: utakatifu wa maisha ya mwanadamu; umuhimu wa familia inayojengeka katika msingi wa uhusiano kati ya Bwana na Bibi wanaokamilishana; tunu ambazo zinapewa kipaumbele cha pekee katika utume wa Askofu mkuu Welby.

Baba Mtakatifu anasema kwa pamoja wanaweza kushirikiana kutafuta haki jamii, kujenga na kudumisha uchumi ambao utatoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi, daima wakipania kutafuta mafao ya wengi na kuendelea kuwa ni sauti ya wanyonge kama kielelezo cha upendo kwa Kristo aliyeonesha upendeleo wa pekee kwa binadamu, lakini leo hii binadamu anaonekana kuwa kama mlaji asiye kuwa na thamani.

Baba Mtakatifu Francisko anatambua kwamba, hizi ni kati ya changamoto ambazo Askofu mkuu Welby anaendelea kuzipatia kipaumbele cha pekee katika utekelezaji wa utume wake sanjari na kupania kuendeleza mchakato wa upatanisho na suluhu ya kinzani mbali mbali ndani ya Jamii. Ni changamoto hii ambayo pia imetolewa na viongozi wa Makanisa nchini Uingereza kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inasaidia upatikanaji wa suluhu ya mgogoro wa kivita nchini Syria; kwa kuhakikisha kwamba, raia wanakuwa salama na uhuru wa kidini unalindwa na kuheshimiwa.

Kama Wakristo wanapenda kushirikisha zawadi ya amani na neema kwa ajili ya dunia, lakini zawadi hizi zinaweza kuzaaa matunda yanayokusudiwa ikiwa tu Wakristo wataishi na kufanya kazi kwa ushirikiano na utulivu na hivyo kuchangia katika hali ya kuheshimiana, amani na utulivu miongoni mwa waamini wa dini na imani tofauti.

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema kwamba, umoja wa Wakristo unaotafutwa unafumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, wanapokutana kama Wakristo watambue kwamba, Kristo yuko kati yao! Huu ni mwaliko wa kufanya hija ya umoja wa Wakristo na udugu ambao unajikita katika upendo unaofanya rejea yake kwa Kristo, ambaye ni maana ya hija hii katika maisha na utume wao!







All the contents on this site are copyrighted ©.