Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 11 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa
Ni kama kawaida tunakutana tena katika viunga vya Radio Vatican kushirikishana pendo
la Mwenyezi Mungu kwa njia ya Neno lake. Ni Dominika ya 11 katika kipindi cha kawaida
cha mwaka C. Mama Kanisa atufundisha Neno la Mungu lenye kuokoa na kuleta msamaha.
Tunasikia
katika somo la kwanza maneno ya faraja toka kwa Mungu kupitia kinywa cha Nathani akimwelekea
Daudi mdhambi “Bwana naye ameiondoa dhambi yako hutakufa” Katika Injili Bwana mwenyewe
Nafsi ya Pili ya Mungu anamwambia mwanamke mkosefu “Imani yako imekuokoa enenda zako
kwa amani”. Basi tokea katika upendo huu ulio mkamilifu Mt Paulo anasema kwa hakika
lazima asulubiwe katika Kristo na Kristo awe hai ndani yake.
Mpendwa msikilizaji,
ujumbe wa Neno la Mungu ni kuishi unyenyekevu na kuomba msamaha vinavyotuletea heri
na baraka tele katika maisha yetu. Mfalme Daudi katika somo la kwanza anaonekana kupokea
msamaha si kwa sababu ya jambo jingine zaidi ya kutamka mbele ya mtumishi wa Mungu
baada ya kutangaziwa uovu wake akisema: “nimekosa mbele ya Mungu” na mara moja baada
ya kusema maneno haya ya toba anapata ondoleo la dhambi. Tendo hili la Mfalme Daudi
latukumbusha pia mfano wa mwana mpotevu, anapoona maji yako shingoni kimbilio lake
ni kuomba msamaha na mara moja anafanyiwa sherehe kubwa pasipo kutarajia.
Mama
amabaye ambaye tumemsikia katika Injili katika mazingira yale alikuwa kahaba na hivi
jumuiya ilimwona kama kinyaa na kama mtu asiyestahili kumgusa Masiha. Katika udhaifu
wa huyu mama na unyenyekevu wa Mungu kunazaliwa msamaha ambao haukutarajiwa machoni
pa Mafarisayo au tuseme walinda sheria. Mama huyu anapomgusa Bwana, mara moja tunaona
anaingia katika safari ya toba inayoambatana na tumaini katika Bwana aliye mkombozi
wake. Mama huyu anapokea furaha ya Yesu mfufuka na anaambiwa imani yako imekuponya.
Gharama
ya msamaha ni imani na kweli imani inaokoa. Mpendwa msikilizaji mara nyingi katika
maisha yetu tunapenda kulipiza na kuadhibu wakosefu na hata kuwatupilia mbali toka
mazingira yetu, lakini leo Bwana anawaleta karibu watoto wake waliowakosefu wakakae
karibu naye. Anathibitisha kuwa kile alichokitangaza aliposoma chuo cha Nabii Isaya
ni kweli katika maisha yake. Nimekuja kwa ajili ya walio maskini (Lk. 4:18).
Basi
mpendwa msikilizaji itikieni wito wa Bwana, mwalikeni maishani mwako kama Mt. Paulo
asemavyo kwangu mimi kuishi ni Kristu, nimesulibiwa katika yeye na maisha yangu yanaendana
na wito wa Mungu wa kutangaza mapendo kwa wadhambi na wema.
Nikutakieni mapendo
na jicho la msamaha katika utumishi na maisha yako yote. Tafakari hii imeletwa
kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.