Makanisa yaendeleze matunda ya majadiliano ya kiekumene kwa kuonesha Mshikamano wa
Kiimani katika Sala na Uinjilishaji
Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani
amewashukuru viongozi wa Kanisa Katoliki ambao kwa takribani kipindi cha miaka hamsini
iliyopita wameonesha namna na jinsi ya kugusa mioyo ya watu kwa njia ya mshikamano
wa upendo, changamoto kwa Wakristo kuchuchumilia umoja miongoni mwao na kwa vile upendo
unaonesha hali tofauti kabisa.
Askofu mkuu Welby anakiri kwamba, ndani mwake
anabeba utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa na Tafakari mbali mbali ambazo
amebahatika kuzipata katika hija ya maisha yake kiasi kwamba, hija yake mjini Vatican
inamfanya kujisikia kuwa yuko nyumbani. Wakristo wanaalikwa kuchuchumilia umoja na
udugu miongoni mwao ili kuendeleza mchakato ulioanzishwa na viongozi wa Makanisa haya
mawili katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita. Ni matumaini yake kwamba, viongozi
hawa wawili watasaidia jitihada za upatanisho kwa ulimwengu na Kanisa.
Wanapaswa
kuendeleza matunda ya majadiliano miongoni mwa Maaskofu, kwa kuonesha mshikamano wa
imani katika sala na Uinjilishaji.Ushuhuda wa umoja na mshikamano utasaidia kukoleza
misingi ya amani na upatanisho, ingawa bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali.
Jambo la msingi ni kujiaminisha kwa Kristo na kwamba, urafiki uliojionesha miongoni
mwao utawasaidia kujenga umoja, kushirikishana mang'amuzi na kusaidia kubeba majukumu
yao, daima wakiwa waaminifu kwa utashi wa Kristo kwa wafuasi wake.
Upendo
wa Kristo uwasaidie kuibeba vyema Misalaba yao na kujifisha, ili kutoa nafasi kwa
Kristo aweze kuishi ndani mwao, kwa kuonesha ukarimu na upendo kwa maskini. Ni changamoto
ya kushikamana ili kukabiliana na vita na madhulumu dhidi ya Wakristo sehemu mbali
mbali za dunia; kusimama kidete dhidi ya Serikali zisizozingatia utawala bora na haki
uchumi, kwani wao kama viongozi ni sauti ya kinabii.