Kukiri dhambi ni kielelezo cha unyenyekevu na unyofu wa moyo!
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kutambua ubinadamu na unyonge wao unaoweza
kuwatumbukiza katika dhambi, ili wawe tayari kupiga moyo konde na kumwendea Yesu Kristo
huku wakiungama dhambi zao kama alivyofanya Mtakatifu Paulo katika hija ya maisha
yake ya imani.
Kuungamana dhambi ni kielelezo cha unyofu na moyo wa unyenyekevu
unaopaswa kuoneshwa kwa namna ya pekee na Makleri, waliopewa dhamana ya kuadhimisha
Mafumbo ya Kanisa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wao kama viongozi wa Kanisa wamepewa
wito na dhamana hii katika chombo cha udongo kama yasemavyo Maandiko Matakatifu.
Msalaba
wa Kristo uwe ni kielelezo cha changamoto ya maisha na utume wao kwa Kristo na Kanisa
lake. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, mwanadamu amekirimiwa ukombozi
kutoka kwa Kristo. Kila mwamini anayekutana na Yesu kwa kutambua udhaifu wake, anakirimiwa
neema ya utakaso na mageuzi makubwa kama ilivyotokea kwa yule Mwanamke Msamaria na
wafuasi wengine wa Yesu.
Baba Mtakatifu Francisko ameyasema hayo Ijumaa, tarehe
14 Juni 2013, wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha
Domus Sanctae Mathae kilichoko mjini Vatican. Ibada hii imehudhuriwa na Viongozi wakuu
na wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Makleri.