Jikiteni zaidi katika: majadiliano, utambuzi na daima muwe mstari wa mbele kutekeleza
wito na utume wenu katika ulimwengu wa utamaduni!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 14 Juni 2013 amekutana na Jumuiya ya Waandishi
wa Jarida la "Civiltà Cattolica" na kuwashukuru kwa mchango, ushirikiano na mshikamano
na Khalifa wa Mtakatifu Petro tangu mwaka 1850 na kuwataka kuendeleza utume wao kwa
kuzingatia mambo makuu matatu: majadiliano; utambuzi na daima kuwa mstari wa mbele
wanapotekeleza utume wao. Baba Mtakatifu anasema Jarida hili linatoa mchango mkubwa
katika majiundo ya watu na kwamba, katika kipindi cha miaka 163 tangu lilipotolewa
kwa mara ya kwanza limepitia mabadiliko makubwa kwa kusoma alama za nyakati. Wanapaswa
kuendelea kuwa waaminifu kwa Kanisa ili kupambana na ukakasi wa mioyo na unafiki unaotokana
na baadhi ya watu kutaka kujifungia katika ubinafsi, dalili za ugonjwa.
Wao
wawe ni madaraja ya majadiliano kati ya waamini na wasioamini ili kutafuta ukweli
ambao kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kutajirishana, kushirikishana
na kujinyenyekeza kama sehemu ya mchango wa majiundo endelevu na mafao ya wengi.
Jumuiya
hii ijitahidi kuzima kiu ya wasomaji wake kwa njia ya mwanga wa Injili kwa kujibu
maswali msingi yanayowatatiza watu wengi kwa nyakati hizi; wawasaidie watu kumwona
Mungu katika maisha na tamaduni zao; Mungu ambaye anaendelea kufanya kazi kwa njia
ya Roho Mtakatifu katika uhalisia wa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu.
Kama
waandishi wa Jarida hili watoe kipaumbele cha pekee katika ukweli, wema na uzuri wa
Mwenyezi Mungu; wasimame kidete kulinda na kutetea maisha ya binadamu na utunzaji
bora wa mazingira, kamwe wasipatwe na kishawishi cha kujitafuta wenyewe, kwani wataugua
na kuzeeka vibaya, changamoto kwao na kwa Kanisa kuendelea kuwa na ari na moyo wa
ujana.
Baba Mtakatifu anawaalika waandishi hao kuwa mstari wa mbele katika
ulimwengu wa utamaduni kwa kuonesha umahiri na mwono halisi wa imani ya Kikristo,
ili Injili iweze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwani, huu ndio utume
halisi wa Wayesuit kuvuka vikwazo na vizingiti ili kuwashirikisha watu Injili ya Kristo.
Wawe ni watu walioko mstari wa mbele.
Anawapongeza kwa mabadiliko makubwa
waliyoyafanya kwenye Jarida hili kwa mwaka huu, kiasi kwamba, linaweza kusomwa hata
kwenye mtandao na watumiaji wa mitandao ya kijamii. Huu ni mwelekeo mzuri unaopaswa
kuendelezwa. Jarida hili linapata chimbuko lake katika maisha na majiundo ya watu,
kila mtu anapaswa kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake na kwamba, anawategemea
katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.