Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Injili ya Uhai Jumapili, tarehe 16 Juni 2013 sanjari
na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni tukio maalum linalopania kuonesha mwanga wa Injili
dhidi ya utamaduni wa kifo unaojionesha katika masuala ya kifo laini, utoaji mimba
na matumizi ya viinitete katika majaribio ya kimaabara.
Ni tukio ambalo Mama
Kanisa anapenda kulitumia kwa ajili ya kutangaza utakatifu wa maisha ya mwanadamu
aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Uhai wa mwanadamu unatishiwa na maendeleo ya
sayansi na teknolojia. Mama Kanisa daima ameendelea kuwachangamotisha waamini na watu
wenye mapenzi mema kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo!
Ni maneno ya
Monsinyo Jean Marie Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji
kwa wahudumu wa sekta ya afya. Anasema, Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili katika maisha
na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alijipambanua kuwa ni mtetezi na mtangazaji
wa Injili ya Uhai inayoendelea kuwekwa rehani kutokana na maendeleo ya sayansi na
teknolojia katika tiba ya mwanadamu. Waraka wa kichungaji wa Injili ya Uhai uliotolewa
na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili ni jibu makini katika kushughulikia changamoto
dhidi ya utamaduni wa kifo.
Magonjwa na mateso ya mwanadamu yanaonekana kuwa
ni mzigo usioweza kubebeka kiasi hata cha kuhatarisha utakatifu na thamani kubwa ya
maisha ya mwanadamu na matokeo yake ni baadhi ya watu kutaka kukumbatia utamaduni
wa kifo! Hapa mwanadamu anashikwa na kigugumizi na kushindwa kutambua kwamba, maisha
yake ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, ameumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu. Maisha ya mwanadamu daima yana uhusiano na uwepo wa Mwenyezi Mungu.
Monsinyo
Mupendawatu anasema, hakuna mtu au serikali yenye mamlaka ya kunyofoa maisha ya mtu!
Sheria zinazokumbatia Eutanasia na utoaji mimba ni kinyume cha Injili ya Uhai. Hiki
ni kishawishi cha binadamu cha kujifanya kuwa ni mmiliki wa hatima ya maisha yake,
jambo ambalo kimsingi si kweli! Vitendo hivi ni mauaji ya makusudi ambayo ni kinyume
cha haki, sheria na utashi wa Mungu kwa binadamu.
Huduma ya tiba kwa mwanadamu
inapaswa kutekelezwa kwa kuongozwa na kanuni maadili, sheria na dhamiri nyofu. Kuna
baadhi ya tiba zilizoendelea zinazotolewa kwa wagonjwa kiasi kwamba, unakuwa ni mzigo
kwa mgonjwa na familia yake, lakini wahudumu wa afya wanaendelea kuitoa wakati mwingine
kwa ajili ya mafao yao binafsi au tafiti wanazofanya! Teknolojia ya kisasa katika
tiba itumike kwa busara na hasa kama kunaonekana kwamba, kuna dalili kwa mgonjwa kuweza
kupata nafuu katika mateso na mahangaiko yake.
Monsinyo Mupendawatu anasema
katika baadhi ya nchi kuna wosia unaotolewa na mgonjwa wa kukataa kula chakula au
kupewa dawa fulani kama njia ya kutema zawadi ya uhai. Hapa Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto wa kumi na sita alionya kwamba, ni kitendo cha mwanadamu kutaka kujikuza
kwa kuelemewa na ubinafsi na uhuru usiokuwa na mipaka. Hapa waamini na watu wenye
mapenzi mema wanapaswa kuwa makini ili kufahamu Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusiana
na mambo ya tiba: Mgonjwa kimsingi ana haki ya kupata chakula, maji na tiba muafaka
kadiri ya hali yake.
Monsinyo Mupendwatu anahitimisha tafakari hii kwa kusema
kwamba, Waraka wa Injili ya Uhai umekuwa ni dira na mwongozo kwa waamini na watu wenye
mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai dhidi ya Utamaduni
wa kifo. Kwa hakika haya ni mapinduzi ya kitamaduni yaliyofanywa na Mwenyeheri Yohane
Paulo wa Pili. Waamini wanapaswa kuendeleza dhamana hii kwa kuwa na majiundo makini
ya dhamiri nyofu inayoheshimu na kuthamini uhai wa binadamu kama zawadi kutoka kwa
Mwenyezi Mungu.