Waziri mkuu wa Slovenia akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 13 Juni 2013 amekutana na kuzungumza na
Bi Alenka Bratusek, Waziri mkuu wa Slovenia na ujumbe wake, waliomtembelea mjini Vatican.
Waziri mkuu baadaye alipata fursa ya kukutana na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu
mkuu wa Vatican pamoja na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya
nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Baba Mtakatifu na mgeni
wake wamejadili pamoja na mambo mengine uhusiano uliopo kati ya Vatican na Slovenia
na kwamba, wameonesha utashi wa kuendeleza ushirikiano huu kwa ajili ya mafao na ustawi
wa Kanisa na Jamii kwa ujumla wake. Wamekubaliana kimsingi kuhusu mchango mkubwa ambao
umetolewa na Kanisa Katoliki nchini humo pamoja na kudumisha uhuru wa kuabudu kwa
ajili ya amani, utulivu na maendeleo ya wananchi wa Slovenia.
Wamegusia pia
changamoto zinazoikabili nchi hiyo kwa sasa na mchango ambao Kanisa linaweza kutoa
katika sekta ya elimu na afya. Masuala ya kimataifa yamejadiliwa pia na viongozi hawa
wawili.