Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwenye
Kikanisa cha Domus Sanctae Mathae mjini Vatican siku ya Alhamisi, amekazia umuhimu
wa kushirikiana na kushikamana miongoni mwa waamini kama njia ya kutekeleza shughuli
ya Uinjilishaji.
Ni mwaliko wa kuheshimiana na kuthaminiana katika hija ya
maisha ya hapa duniani, kama Kristo mwenyewe alivyojinyenyekeza akawa mtii hata kufa
Msalabani, kiasi cha kuwajalia wafuasi wake ile dhamana ya kuwa ni ndugu zake wapendwa.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutumia vyema ndimi zao, kwani ulimi ni
kiungo kidogo sana katika mwili wa mwanadamu, lakini kinaweza kusababisha madhara
makubwa katika maisha ya watu. Ndiyo maana Mwenyezi Mungu amemwekea mwanadamu amri
ya kutosema uongo, ili kujengana na kuimarishana katika mambo mema. Waamini wajenge
fadhila ya unyenyekevu, wakiongozwa na sheria ya upendo kwa Mungu na jirani; wasimame
kidete kulinda na kutetea haki na amani.
Baba Mtakatifu amewapongeza wananchi
wa Argentina wanaoishi na kufanya kazi zao hapa mjini Roma kutokana na mchango wao
kwa maendeleo na ustawi wa Argentina. Ibada ya Misa Takatifu imehudhuriwa na Balozi
wa Argentina nchini Italia ambaye pia ni mwakilishi wa FAO.
Papa anawataka
waamini kuendelea kujishikamanisha na sheria ya Mungu ambayo Kristo mwenyewe ameipatia
utimilifu wake. Ili kujenga na kuimarisha mahusiano mema, kuna haja kwa waamini kuendelea
kufanya toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu anawalika waamini kuwapenda na kuwaheshimu
jirani zao, kwa kuwatakia mema!