2013-06-13 11:25:08

Makanisa yanapania kuona kwamba, tunu ya maisha, haki na utu wa mwafrika vinadumishwa


Shirikisho la Mabaraza ya Makanisa Barani Afrika linaadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu lilipoanzishwa nchini Uganda kunako mwaka 1963, wakati ambapo nchi nyingi za Kiafrika zilikuwa zinajitwalia uhuru wake wa bendera. Kilikuwa ni kipindi cha mapambano, kinzani na mikakati ya kuondokana na ujinga, umaskini na magonjwa kwa kuhakikisha kwamba, Bara la Afrika linatumia rasilimali zake kikamilifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wake.

Mkutano wa kumi wa Shirikisho la Mabaraza ya Makanisa Barani Afrika uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu "Mungu wa uhai, liongoze Bara la Afrika katika haki, amani na utu", ulikuwa ni fursa kubwa kwa wajumbe kuchangia kwa kina na mapana umuhimu wa tunu hizi kwa ajili ya mchakato wa maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili Barani Afrika.

Itakumbukwa kwamba, maadhimisho haya kikanda ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni utakaofanyika kuanzia tarehe 30 Oktoba hadi tarehe 8 Novemba 2013 mjini Busan, Korea ya Kusini.

Askofu mkuu Valentine Mokiwa, Mwenyekiti wa Shirikisho la Makanisa Barani Afrika amesema kwamba, kuanzishwa kwa Shirikisho hili kulipania kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, tasaufi ya Kiafrika inamwilishwa katika masula ya: kijamii, kisiasa, kimaadili na kiutu ili kuleta mabadiliko yaliyokuwa yanakusudiwa Barani Afrika baada ya kuanguka kwa ukoloni na kuanza kuibuka kwa ukoloni mamboleo.

Askofu mkuu Mokiwa anawataka wajumbe wa Shirikisho kuendelea kusimama kidete kupambana na baa la umaskini kwani hii ni dhambi na kashfa katika Karne ya ishirini na moja.

Kwa upande wake, Dr. Olav Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ameyataka Makanisa Barani Afrika kushikamana kwa dhati na kuendelea kuwa ni sauti ya wanyonge dhidi ya ukosefu wa haki msingi na vitendo vya uvunjifu wa misingi ya amani na utulivu.

Bara la Afrika lina utajiri mkubwa wa rasilimali na maliasili, lakini kwa bahati mbaya, utajiri wote huu kwa miaka mingi umeendelea kuwanufaisha watu wachache katika Jamii wakati ambapo kuna mamillioni ya watu wanateseka kwa baa la njaa, magonjwa na umaskini. Hii ni changamoto ya kusimama kidete kutetea haki ya kiuchumi, jambo linaloungwa mkono na Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Kuna haja ya kubadili mwelekeo wa sasa ambao umeligeuza Bara la Afrika kuwa ni mpokeaji wa misaada kutoka nje na badala yake liwe ni mdau wa shughuli za kiuchumi ili kujenga na kuimarisha haki, amani na utu!

Baadhi ya wajumbe wamesema kwamba, kuna haja kwa Makanisa kuwekeza kwa vijana na wanawake Barani Afrika ili waweze kushiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika, kwa kuchangia kwa hali na mali karama na mapaji ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu, yanayopaswa kutumiwa kwa ajili ya mafao ya wengi.

Vijana wa Kiafrika wajiamini na kujiwekea mikakati ya maendeleo badala ya kuingiwa na kishawishi cha kutaka kuzamia ughaibuni kwa kudhani kwamba, huko kuna kula kuku kwa mirija, lakini wanapofika Ughaibuni wanakumbana na adha ya maisha na hali ya kukata tamaa! Ni mwaliko kwa Serikali Barani Afrika kukomesha ajira za watoto wadogo hasa huko Sierra Leone, DRC na baadhi ya nchi za Kiafrika.

Nchi nyingi za Kiafrika zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara zimefanya maboresho katika misingi ya demokrasia na utawala bora; zinaendelea kupembua kuhusu mikataba pamoja na kufanya maboresho katika huduma za kijamii hususan katika sekta ya elimu na afya.







All the contents on this site are copyrighted ©.