2013-06-13 09:02:11

Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa kufanyika mjini Cebu, Ufilippini, Januari 2016!


Kardinali Tarcisio Bertone Katibu mkuu wa Vatican anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kauli mbiu ya Maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa litakalofanyika mjini Cebu, nchini Ufilippini kunako mwaka 2016. Maadhimisho haya yatafanyika kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 31 Januari 2016 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu" Wakolosai 1: 27.

Uchaguzi wa mahali ambapo Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa lingefanyika ulitolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake kwa njia ya video wakati wa kufunga Maadhimisho ya Kongamano la 50 la Ekaristi Takatifu Kimataifa lililofanyika mjini Dublin, mwezi Juni 2012.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliwasihi waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Ufilippini kuanza maandalizi mara moja kwa ajili ya maadhimisho haya, kama sehemu ya mchakato wa kupyaisha maisha ya Kikristo nchini humo na kwa wale wote watakaoshiriki kwa namna mbali mbali.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ufilippini kwamba, Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu kimataifa nchini mwao, itakuwa ni fursa makini katika jitihada za kukuza na kuimarisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu nchini humo sanjari na Maadhimisho ya Miaka 500 tangu walipoinjilishwa kwa mara ya kwanza.

Hii ni changamoto ya kudumisha mchakato wa Uinjilishaji, ari na moyo wa kimissionari ili kumshuhudia Kristo kwa kina na mapana zaidi. Maadhimisho haya yatakuwa ni zawadi kubwa kwa vijana Barani Asia kutambua dhamana na wito wao katika azma ya uinjilishaji wa kina.







All the contents on this site are copyrighted ©.