2013-06-13 09:41:25

Jitokezeni kuenzi zawadi ya uhai!


Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni changamoto kwa waamini kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, kwani ni kwa njia ya kuamini, waamini wanaweza kupata maisha tele! Ni changamoto endelevu inayotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland mara baada ya kuhitimisha mkutano wao wa mwaka hivi karibuni.

Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za Mama Kanisa katika kulinda na kutetea Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi kifo kinapomfika kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu. Kwa namna ya pekee, Mama Kanisa ataadhimisha tukio hili mjini Vatican kwa kuungana na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumamosi tarehe 15 na kilele chake kitakuwa katika Ibada ya Misa Takatifu Jumapili, tarehe 16 Juni 2013 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kauli mbiu iliyochaguliwa katika Maadhimisho haya inaonesha jinsi ambavyo Kanisa linapania kulinda na kudumisha utu, heshima na maisha ya binadamu. Ibada hii ni kwa ajili ya kuenzi wale wote ambao wanapenda kuunga mkono juhudi za Kanisa katika kutetea na kutangaza Injili ya uhai, kama alivyofanya Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili kunako tarehe 25 Machi 1995 alipochapisha Waraka wa Kichungaji, Injili ya Uhai, dira na mwongozo kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kupinga kwa nguvu zao utamaduni wa kifo!

Baraza la Maaskofu nchini Ireland limeonesha nia na utashi wa kuendeleza huduma ya hali na mali pamoja na utoaji wa ushauri nasaha kwa wale walioathirika kutokana na nyanyaso za kijinsia walizofanyiwa na baadhi ya viongozi wa Kanisa, kama njia ya kukuza na kudumisha haki.

Maaskofu wa Ireland wanapenda kuwakaribisha viongozi wa G8 watakaofanya mkutano wao mkuu hapo tarehe 17 hadi 18 Juni 2013 mjini Enniskillen, kwa kuwataka kutambua na kuthamini mshikamano wa kimataifa unaoongozwa na kanuni auni kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na hali ngumu ya uchumi duniani; magonjwa, ujinga na baa la njaa linaloendelea kuwakumba maelfu ya watu duniani.

Wananchi wengi wamekata tamaa kutokana na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo, kumbe, kuna haja kwa viongozi wa G8 kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kuwajengea tena wananchi matumaini katika maisha yao. Wamekazia ukweli na uwazi katika masuala ya fedha na kodi na kwamba, nchi maskini wanapaswa kufaidika na utajiri wa rasilimali za nchi zao kwani hii ni haki yao msingi.

Maaskofu wanasema kwamba, ni kashfa kubwa kwa sasa kuona watu wanaendelea kuteseka kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha wakati dunia imeonesha mabadiliko na maendeleo makubwa katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia. Ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kupambana kufa na kupona ili kurekebisha mifumo tenge inayoendelea kusababisha ukosefu wa haki msingi duniani.

Viongozi wa Kimataifa wanapaswa pia kutekeleza ahadi zao ili kufanikisha Malengo ya Maendeleo ya Millenia Kimataifa ifikapo mwaka 2015. Mageuzi ya biashara na soko la kimataifa; udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi na matumizi mabaya ya nishati uoto ni kati ya mambo ambayo yanapaswa kujadiliwa kwa ukweli na uwazi ili kujenga na kudumisha haki jamii, amani na mshikamano wa kimataifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki linaendelea kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 itakayofanyika mjini Rio de Janeiro kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013 kwa kuongozwa na kauli mbiu "basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi". Askofu mkuu Diarmuid Martin wa Jimbo kuu la Dublin ataongoza ujumbe wa Baraza la Maaskofu unaowajumuisha vijana 165 kwenda kwenye Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Vijana watakaobaki nchini Ireland watafanya maadhimisho kwenye Majimbo yao kadiri ilivyopangwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland limefanya kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Maadhimisho ya Kongamano la 50 la Ekaristi Takatifu Kimataifa lilipoadhimishwa mjini Dublin na kwamba, walipata nafasi ya kutafakari kwa mara nyingine tena nyaraka za Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Maaskofu wanawashukuru sana waamini na watu wenye mapenzi mema waliochangia kwa hali na mali ili kufanikisha tukio hili la kiimani. Maaskofu wanawaalika waamini kufanya uchambuzi yakinifu ili kubainisha urithi unaojikita katika Maadhimisho ya Kongamano la 50 la Ekaristi Takatifu Kimataifa.

Mwishoni, Maaskofu wamezungumzia kuhusu mgogoro wa Syria na athari zake na kwamba, wanapenda kuonesha mshikamano wao wa dhati na wale wote walioguswa na vita inayoendelea nchini humo. Wamekazia umuhimu wa Sakramenti ya ndoa na Familia katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, hii ni mada itakayofanyiwa kazi mwezi septemba mwaka huu.







All the contents on this site are copyrighted ©.