2013-06-13 07:37:56

Endelezeni majadiliano ya kidini kwa njia mshikamano, mkiheshimiana na kuthaminiana pamoja na kutolea ushuhuda wa imani ya Kikristo


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, Jumatano tarehe 12 Juni 2013, majira ya usiku amekutana na kusali na Familia ya Mungu kwenye Kanisa la Bikira Maria mjini Dubai, Falme za Kiarabu, tukio ambalo anasema, ni kama siku ile ya Pentekoste watu kutokana kila pembe ya dunia walipokuwa wamekusanyika mjini Yerusalem, wote wakasikilizana.

Katika mahubiri yake, Kardinali Filoni amekazia umuhimu wa kazi kwa ajili yao binafsi na familia zao, changamoto ya kuendeleza majadiliano ya kidini kwa njia ya mshikamano; kwa kuheshimiana na kuthaminiana pamoja na kutolea ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kutambua kwamba, wanaishi na kufanya kazi katika Jamii inayoundwa na idadi kubwa ya Waamini wa dini ya Kiislam.

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu na Ibada mbali mbali iwe ni fursa ya kuwaunganisha na kuwaimarisha katika misingi ya imani ya Kikristo kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu pamoja na jirani. Ni mwaliko pia wa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha katika maisha yao Sheria ya Mungu ambayo imefunuliwa kwa utimilifu wake na Yesu Kristo anayewataka wafuasi wake kumpenda Mungu na jirani kama utimilifu wa sheria.

Watambue kwamba, wameumbwa na Mungu na kukombolewa kwa damu Azizi ya Kristo inayowafanya kuwa ni viumbe wapya wanaoshiriki ule mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, kwani wao pia ni watoto wateule wa Mungu wanaoweza kumwendea kila wakati wanapotumbukia katika dhambi ili awaonjeshe upendo na huruma yake unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba.

Kardinali Filoni anawaambia Waamini wa Kanisa Katoliki wanaoishi na kufanya kazi mjini Dubai kwamba, wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili kushinda kishawishi cha kumezwa na tamaduni na imani za watu wengine. Wawe waaminifu katika maisha ya ndoa, sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na matendo ya huruma. Katika mazingira magumu kama wanayokabiliana nayo, kishawishi kikubwa kinaweza kuwa ni kile cha kubadili dini ili kurahisisha mambo.

Yesu daima anaendelea kubisha hodi katika milango ya mioyo yao, wakiwa tayari wanaweza kumfungulia na kuendeleza maisha yao ya Kikristo, huku wakiandamana na Yesu, kwani yeye ni njia, ukweli na uzima. Watambue kwamba, hawana tofauti na watu wengine, wanaishi duniani, lakini wao si wa dunia hii, hatima ya maisha yao ni mbinguni, kumbe bado ako safarini huku wakiendea taji lisilochakaa kamwe!







All the contents on this site are copyrighted ©.