2013-06-12 10:32:31

Watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi ni matokeo ya biashara haramu ya binadamu!


Biashara haramu ya binadamu ni kati ya sababu kubwa zinazopelekea watoto wengi kujikuta wanaoishi katika mazingira hatarishi na matokeo yake wanakumbana na nyanyaso na madhulumu ya kila aina. Ni watoto ambao wanaathirika tangu wakiwa wadogo na hivyo kuwa ni tishio kwa Jamii kwa siku za usoni.

Kuna baadhi ya watoto ambao kutokana na kumong'onyoka kwa misingi ya maadili na utu wema, wakajikuta wakiacha masomo kutokana na sababu mbali mbali na matokeo yake sasa wanaishi kwenye mazingira magumu, licha ya wazazi na walezi wao kuwapatia fursa ya kusoma.

Haya ndiyo yanayoendelea kujitokeza nchini Sierra Leone, Afrika Magharibi, ambako biashara haramu ya binadamu inafanywa hata na ndugu na jamaa wa karibu kwa madai kwamba watakapofika mjini watawapatia elimu bora na ajira itakayowajengea uwezo wa kusaidia familia zao kijijini. Lakini wanapofika mjini Freetown, mambo yanabadilika na kujikuta wanafanyishwa kazi kama watumwa majumbani au kutumbukizwa na kutekelezwa kwenye biashara haramu ya ngono.

Uchunguzi wa kina uliofanywa kunako mwaka 2010 unaonesha kwamba, kuna zaidi ya watoto 2,500 wanaolala kwenye mitaa ya Mji wa Freetown kila siku, hali inayopelekea nyanyaso na madhulumu kwa watoto hao. Ni mashirika machache yasiyo ya Kiserikali ambayo yameanzisha mchakato wa kuwakusanya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ili kuwarudisha kwenye familia zao, jambo ambalo si rahisi hata kidogo. Kuna haja kwa Jamii kusimama kidete kulinda na kutunza utu na heshima ya watoto hawa!







All the contents on this site are copyrighted ©.