2013-06-12 08:02:34

Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wanahitaji faraja, upendo, huruma na kusaidiwa ili kuondokana na hali hii!


Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kunako mwaka 2012 liliendesha mkutano wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi Barani Afrika. Mkutano huu uliwashirikisha wajumbe 88 kutoka ndani na nje ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM. RealAudioMP3

Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, ni kati ya wajumbe waliohudhuria mkutano huu uliofanyika kwenye Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Jijini Dar es Salaam. Anasema, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wanahitaji faraja na upendo kutoka kwa wadau mbali mbali. Hawa ni matokeo ya mtu binafsi, kumong'onyoka kwa misingi ya maadili, utu wema na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni watoto wanaokabiliana na hatari nyingi katika maisha yao.

Askofu Msonganzila anaendelea kusema kwamba, kinzani, migawanyiko na mafarakano katika familia; baadhi ya watu kushindwa kuzingatia: tamaduni,mila na desturi njema za Kiafrika ni kati ya mambo ambayo yamepelekea kwa watoto wengi kujikuta wakiiishi nje ya mipaka ya maisha na tunu za kifamilia; hawa ndio watoto wale wanaoishi katika mazingira hatarishi. Baadhi yao wamekuwa na ndoto ya kutaka kupata maisha ya hali ya juu bila kuwa na maandalizi ya kina wala kipato. Ni watoto ambao wamejikuta wakijitumbukiza na kutumbukizwa katika matumizi haramu ya dawa za kulevya; ukahaba na kazi za shuruti.

Askofu Michael Msonganzila anasema, watoto hawa wanapaswa kusaidiwa ili kupambana na hali yao ya maisha, kama ilivyotokea kwa wale wanafunzi wa Emmaus waliokuwa wakisafiri kutoka Yerusalem kwenda Emmaus wakakutana na Yesu ambaye aliwafafanulia kuhusu utajiri uliofumbatwa kwenye Maandiko Matakatifu. Kumbe, Neno la Mungu linapaswa kuwa ni dira katika kujitambua, kuchambuliwa na kuchambuana; ili waamini waweze kulipokea, kulikubali na kulimwilisha katika maisha na vipaumbele vyao.

Wadau mbali mbali katika malezi na makuzi ya watoto wanatambua kwamba, watoto hawa wanahitaji kuonjeshwa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, hata katika mazingira haya hatarishi, kwani pengine hawa ni matokeo ya dhambi jamii; athari za uchumi, kinzani na migogoro ya kifamilia na kijamii; kisiasa na kielimu. Watoto hawa wanahitaji kupendwa na kuthaminiwa kama alivyofanya Msamaria mwema.

Jamii ioneshe huruma pamoja na kuibua mbinu mkakati wa kuwasaidia ili waweze kuondokana na hali yao mbaya. Inasikitisha kuona na kusikia kwamba, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wanatumiwa pia kwa ajili ya kuendeleza biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na ukahaba, mambo ambayo yanaendelea kuwadidimiza na kuwaangamiza.

Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma anasema, nchi nyingi za Bara la Afrika zimekuwa ni soko na njia za biashara haramu ya binadamu, changamoto kwa vyombo vya ulinzi na usalama kujipanga vyema ili kuzuia na kudhibiti biashara hii haramu inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Haya pia ni mambo ambayo yanajadiliwa katika Maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.